NA FATUMA KITIMA, DAR ES SALAAM

TANZANIA imekabidhi Uenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), kwa nchi ya Msumbiji baada ya kumaliza muda wake wa mwaka mmoja.

Akizungumza jana kwenye mkutano uliofanyika katika ukumbi wa kituo cha kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Katibu wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Wilbert Ibuge, alisema kuwa ndani ya mwaka mmoja Tanzania imeongeza na kupitisha mpango mkakati na dira ya SADC hadi mwaka 2050.

Balozi Ibuge alisema kuwa tangu Tanzania ilipokabidhiwa nafasi ya Uenyekiti wa SADC imeifikisha jumuiya hiyo mahali ilipotakiwa.

Alitaja mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha kushika nafasi ya Uenyekiti Tanzania ni pamoja na kupitisha bajeti ya utekelezaji wa mpango kazi licha ya kuibuka kwa ugonjwa wa COVID 19.

Aidha alisema mbali na janga la ugonjwa wa Covid 19, serikali katika nchi za SADC zimeweza kuweka utaratibu wa kusafirisha bidhaa kipindi cha janga hilo.

Pia alisema Tanzania imeweza kujitangaza katika sekta za kiuchumi na kiutalii tangu kukabidhiwa kuwa Mwenyekiti.

Naye Balozi wa Msumbiji, Monica alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli kwa kuongoza vyema SADC tangu ilipochaguliwa mwaka jana.

“Tunapenda maendeleo ya uchumi hivyo tumefurahi na tunachukua nafasi hii kuwa Mwenyekiti wa SADC,” alisema