Serikali yasema ililipa deni lote kwa Exim
NA KHAMISUU ABDALLAH
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar, imesema fedha za mkopo mradi wa ujenzi wa Taminal III zilizotolewa na benki ya Exim ya nchini China zitalipwa kwa mujibu wa makubaliano ya pande mbili.
Waziri wa Fedha na Mipango, Balozi Mohammed Ramia Abdiwawa, alieleza hayo jana alipofanya ziara ya kuangalia maendeleo ya ujenzi wa jengo la terminal III.
Alisema hadi mwezi Julai mwaka huu tayari vipengele 11 kati ya 25 na kwamba mwezi Juni mwaka 2022 serikali itakuwa imeshalipa mkopo wote inaodaiwa na benki hiyo.
Aidha alisema mwezi Septemba mwaka 2019 serikali ilidhamiria kukamilisha ujenzi huo kwa mara ya mwisho na kampuni ya BCEG kupitia pesa za mkopo kutoka Benki ya Exim ambapo dola milioni 58 zilitiwa saini ili uweze kukamilika.
Alisema uwanja huo utakapomalizika utakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria milioni 1.6 kwa mwaka.
Hata hivyo, alisema kukamilika kwa uwanja huo kutainua uchumi wa Zanzibar kupitia sekta za biashara hasa sekta ya utalii kwa wageni wa nje ya nchi. “Serikali lengo letu kuwa uwanja huu unakuwa na umuhimu mkubwa hasa katika kutupatia mapato ya kutosha”, alisema.
Mbali na hayo aliipongeza wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji katika kusimamia ujenzi huo na kulitekeleza vyema jukumu walilokabidhiwa na wanalifanya kwa uzalendo.
Mbali na hayo alisema mwezi huu, serikali inapokea vifaa vya mwisho kutoka nje kwa ajili ya jengo hilo ikiwemo viti na vifaa vyengine.
“Lengo letu la kufanya ziara hii ni kuangalia pesa tunazozitoa zinatumika kama ilivyokusudiwa, kwa kweli sina mashaka pamoja na kujitokeza kwa maradhi ya corona tumefikia hatua nzuri”, alisema.
Mbali na hayo aliipongeza kampuni ya BCEG kwa hatua inazozichukua kuhakikisha ifikapo mwezi Septemba mwaka huu uwanja huo wanaukabidhi serikalini.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Mustafa Aboud Jumbe, alisema serikali ilikuwa inalipa dola milioni moja kila mwezi kwa miezi 10 iliyolipwa na kunzia mwezi Agosti mwaka huu imeanza kulipa dola milioni mbili kwa mwezi.
Meneja wa mradi huo, Yasser de Costa alisema tayari zaidi ya asilimia 85 imeshafikiwa katika ujenzi huo na kuahidi kuwa ifikapo mwezi Septemba mwaka huu watakabidhi jengo hilo serikalini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed Shein anatarajiwa kuwa mgeni ramsi katika ufunguzi wa awali wa uwanja huo Septemba 22 mwaka huu.