LONDON,UINGEREZA

SHIRIKA  la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) limetangaza kuwa,theluthi moja ya watoto duniani watashindwa kupata elimu katika kipindi hiki cha maambukizi ya virusi vya corona.

Ripoti iliyotolewa ya UNICEF ilisema kuwa,theluthi moja ya watoto wanaokwenda skuli duniani yaani karibu watoto milioni 500 hawakuweza kupata elimu katika kipindi kilichofungwa skuli kutokana na maambukizi ya corona.

Ripoti ya UNICEF ilisema kuwa, katika kilele cha utekelezaji wa sheria kali za kuzuia watu kutoka nje kote duniani watoto bilioni 1.5 wenye umri wa kwenda skuli waliathiriwa.

Maambukizi ya virusi vya corona kote duniani na kutokuwepo chanjo na dawa mujarabu ya kutibu ugonjwa wa COVID-19 kumezilazimisha nchi mbalimbali kuchukua hatua za dharura zinazohusiana na masuala ya afya ikiwa ni pamoja na kufungwa skuli,masomo na maeneo ya kazi.

Tamwimu zinaonesha kuwa, hadi sasa watu zaidi ya milioni 24 wameambukizwa virusi vya corona kote duniani na wengine zaidi ya laki nane na 30 elfu walifariki dunia kutokana na virusi hivyo.