AGOSTI 29 mwaka 1949, USSR ilikuwa rasmi taifa linalomiliki silaha za atomiki kwani ilifanikiwa kuripua bomu lake la kwanza la majaribio la nyuklia lililojulikana kama RDS-1.

Serikali za magharibi zilishitushwa sana suala hilo kwa mujibu wa rekodi za shirikia la ujasusi la Marekani CIA, majasusi wa Marekani walifikiria Wasovieti wasingeweza kutengeneza bomu la nyuklia kabla ya mwaka 1953.

Cha kushangaza ni kwamba ni mwanasayansi wa Marekani, Theodore Hall, ndiye aliyeisaidia Moscow kufikia azma yake ya kumiliki silaha za nyuklia kwa kuipatia Usovieti teknolojia na taarifa muhimu za nyuklia.

Ni kweli kwamba Theodore Hall hakua raia wa pekee wa Marekani aliyevujisha siri ya uundaji wa bomu la atomiki kwa maadui wa nchi hiyo, lakini kilichompatia umaarufu ni jinsi alivyoweza kutekeleza kazi yake kwa siri kubwa bila kutambuliwa.

Theodore Hall ni mzaliwa katika jiji la New York, aliyesomea sayansi ya nyuklia katika chuo kikuu cha Harvard, ambaye baadae aligeuka na kuwa jasusi wa Usovieti.

Kwa hakika haikuwa jambo la kushangaza kuwa bomu la RDS-1 lilifanana sana na bomo la atomiki lililorushwa na Marekani pale ilipoushambulia mji wa Nagasaki uliopo nchini Japan mnamo Agosti 9 mwaka 1945.

Taarifa za kina kuhusu muundo wa bomu hilo ilifichuliwa kwa Wasovieti kutoka kwa msiri wa ndani wa mradi wa Manhattan, lilitotomiwa kuelezea mpango wa uundaji wa silaha za atomiki uliokuwa unaongozwa na Washington, kwa ushirikiano na Uingereza na Canada.

Kuweka siri ilikuwa kigezo kikubwa. kulingana na nukuu ya taarifa iliyochapishwa katika jarida la ‘life magazine’ la mwaka 1945, “Bila shaka ni watu wachache sana kote nchini Marekani waliojua maana halisi ya mradi wa Manhattan”. Mmoja wa watu hao alikuwa Theodore Hall.

Alizaliwa Oktoba 20 Mwaka 1925, mama yake mzazi alikua mke nyumbani na baba yake alikua mfanyabiashara. Hall aliishi nyakati ngumu sana kimaisha kwa Wamarekani wa kawaida.

Lakini hali hiyo haikumzuia Hall kufikia malengo yake kimasomo hasa katika somo la hisabati na fizikia. Akiwa na umri mdogo wa miaka 16, alipata nafasi ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Harvard.

Uwezo wake wa kimasomo uligunduliwana maofisa wa Marekani waliokuwa wakitafuta watu watakawaofanyia kazi katika mradi mpya wao nyuklia. Theodore Hall alihojiwa na kupewa nafasi ya kuhudumu katika maabara ya kisiri ya Los Alamos mwanzoni mwa mwaka 1943.

Lakini kile ambacho maofisa wa Marekani hawakufahamu ni kuwa mwanafizikia huyo mchanga alikuwa amefanyiwa usaili mwingine kama huo.

Hall alikuwa mwanachama wa kundi la wanafunzi wa Harvard wanaoegemea falsafa ya Karl Marx akiwa na mwanafunzi mwenzake aliyefahamika kama Saville Sax.

Sax alikuwa mwana wa kiume wa wahamiaji wa Urusi na alikuwa mfuasi sugu wa Kikomunisti japo alizaliwa na kulelewa mjini New York. Ukweli ni kuwa Sax ndiye aliyemshawishi Theodore Hall kujiunga na Wasovieti na kuwa ajenti wa kutoa siri za nyuklia kwa Wasovieti.

Mwezi Disemba mwaka 1944, Hall kwa ushirikiano na mwanafunzi mwezake wa zamani, walivujisha kwa mara ya kwanza kabisa siri kubwa kutoka Los Alamos – iliyohusisha namna ya kuunda bomu la plutoniki.

“Wakati huo mwaka 1944, Nilikuwa na hofu kuhusu hatari ya Marekani kuwa mmiliki pekee wa silaha za atomiki baada ya vita vya dunia,” Theodore Hall alisema katika taarifa iliyoandikwa na kuchapishwa na Gazeti la New York Times mwaka 1997, miaka miwili kabla kufariki dunia kutokana na saratani ya figo.

Hall alidai kuwa USSR kumiliki ni njia bora zaidi ya kuidhibiri Marekani. “Muungano wa Sovieti wakati huo haukuwa adui, bali mshirika wa Marekani.” Hall alisema, “Wasovieti walipigana na Wanazi kishujaa, hatua ambayo huenda iliisaidia washirika wake wa Magharibi kutoshindwa.”

Alijulikana na Wasovieti kama “The Youngster” na aliendelea kuifichulia Moscow siri kuhusu teknolojia ya mawasiliano, hasa jinsi ya kulipua mabomu yalioundwa kwa madini ya plutoniam.

Bomu lililodondoshwa na Marekani katika mji wa Nagasaki nchini Japan liliundwa kutokana na madini ya plutonium-tofauti na lile lililolenga Hiroshima, ambalo liliundwa kutokana na madini ya uranium.

Marekani na USSR huenda walipigana dhidi ya adui mmoja wakati wa vita vikuu vya pili vya dunia, lakini huenda hatua hiyo haikuizuia Moscow na Washington kuchunguzana.

Ukweli wa mambo ni kuwa Marekani katika hatua ya kukabiliana na ujasusi wa Wasovieti ilianzisha mradi uliofahamika kama Venona ambao ulianza kazi mwezi Februari mwaka 1943.

Mwezi Disemba mwaka 1946, majesusi wake walifanikiwa kudukua mawasiliano kutoka NKVD, wizara wa ya mambo ya ndani ya Muungano wa Sovieti.

Mawasiliano ya Wasovieti iliyodukuliwa na Marekani yalibaini kuwa Wasovieti wamekuwa wakichunguza kisiri mradi wa Manhattan.

Theodore Hall alikuwa akifanyia kazi mradi wake wa PhD katika Chuo Kikuu cha Chicago mwaka 1950, wakati maofisa wa upelelepezi wa Marekani FBI walipomgongea mlango.

Jasusi mwingine wa Los Alamos, alikuwa mwanafizikia wa Ujerumani Klaus Fuchs, ambaye alikamatwa mwaka uliotangulia, baada ya kukiri jukumu lake katika kuwatumia maadui wa siri za nyuklia za Marekani.

Hata hivyo, wapelelezi wa FBI hawakupata ushahidi wowote kutoka kwa Theodore Hall na Saville Sax, ambaye pia alichunguzwa uliothibitisha kuwa walifichua siri kwa Moscow.

Wanasayansi hao hawakupatikana na madai ya kutoa siri kwa Urusi kwa sababu uchunguzi haukuonesha ushahidi kwa sababu Hall hakujihusisha na masuala hayo baada ya mradi wa Manhattan.

Kulikuwa na nyaya za Moscow za mawasiliano ya Moscow ambazo zilitumika kama ushahidi, lakini mamlaka ya Marekani hazikutaka kuzitumia mahakamani, kwa sababu hatua hiyo ingelifichua kuwa walidukua mawasiliano ya Wasovieti.

Mwisho wa siku, Hall aliponea mashtaka na wala hakuchukuliwa hatua kama watu wengine waliofungwa jela na na wengine kunyongwa kwa kutoa siri za nchi.

Licha ya hayo Hall na mke wake walihofia usalama wao. Aliachana na wadhifa wake wa kielimu mjini Chicago na kuangazia shughuli za utafiti katika hospitali za New York.

Mwaka 1962, alipata kazi katika Chuo Kikuu cha Cambridge hali iliomfanya kuhamia Uingereza na mke wake. Theodore Hall alistaafu mwaka 1984 na kuamua kuishi maisha ya kisiri.

Lakini mwaka 1996, mambo aliyofanya zamani yalifichuliwa baada ya mawasiliano kati yake na Urusi kutolewa hadharani. Wakati huo mashahidi wote waliofahamu mienendo ya Hall walikua wamefariki dunia akiwamo Savile Sax.

”Inadaiwa kuwa niligeuza mkondo wa historia,” Hall aliwaambia waandishi wa New York Times.

“Pengine kama mkondo wa historia haukugeuzwa huenda mngeliongoza vita vya silaha za atomiki kwa miaka 50, Kwa mfano bomu hilo lingelidondoshwa China mwaka 1949 ama mwanzoni mwa miaka ya 1950.”

“Kwa kweli kama nilifanikiwa kubadili matukio hayo, Nakiri makosa,” alisema.

Hakujawahi kuwa na mashambulio ya nyuklia tangu yalipofanyika mashambulio ya Hiroshima na Nagasaki miaka 74 iliopita na Theodore Hall alifariki akiamini kuwa alichangia kutotumika tena kwa silaha hiyo ya maangamizi.