NA JAFFAR ABDALLA, PEMBA
VIONGOZI wa klabu zinazoshiriki ligi daraja la kwanza taifa Pemba, wametishia kugoma, endapo ligi hiyo haitochezwa kwa mizunguruko miwili kama kanuni ya mashindano hayo inavyoelekeza.


Walieleza kuwa kuna tetesi za chini kwa chini, kuwa ligi daraja la kwanza itachezwa kwa mzunguruko mmoja, kwa kumalizia michezo iliyobakia baada ya kusimama kwa muda kupisha janga la corona lililoikumba dunia.


Wakizungumza kwenye kikao cha kujadili juu ya mustakbali wa ligi hiyo, huko uwanja wa Gombani, walisema iwapo Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), litaendesha mashindano hayo kwa mzunguruko mmoja klabu hazitoshiriki ligi hiyo.


Msemaji wa timu ya Yonger Islander Muhamed Hatibu(Kishore), pamoja na kocha wa New star Hamis Hamadi, walisema kama ligi hiyo itashindwa kuchezwa kwa mikondo miwili vyema ikafutwa na aliye juu apandishwe daraja na kusisitiza hakuna kushuka kwa klabu yoyote.
“Sisi viongozi wa klabu za Pemba, msimamo wetu ni kwamba kama ligi hiyo itashindwa kuchezwa kwa mizunguruko miwili, basi ni bora ifutwe na iliye juu apewe haki yake vyenginevyo hatutoshiriki ligi”walisema.


Kwa upande wake kocha wa timu ya Kizimbani Juma Ali Salum, alisema ZFF ndio iliyosababisha kuchelewa ligi hiyo, kwa kitendo cha kutokuwalipa waamuzi mafao yao ya muda mrefu na waamuzi kuamua kudai haki zao kwa njia ambazo waliona zinafaa.


Alisema licha ya kuwa ligi hiyo iliingiliwa na janga la corona na kulazimika kusimama kwa muda, lakini ZFF ilizorotesha michezo, kitendo kilicho wafanya waamuzi kuingia mitini kwa baada ya kutopewa mafao yao.