NA NASRA MANZI

KOCHA wa timu ya Rio De Janairo inayoshiriki ligi daraja la tatu Wilaya ya Magharibi ‘A’ Unguja Mohamed Omar, ameiomba Serikali pamoja na Shirikisho la mpira wa miguu Zanzibar  (ZFF)  kusaidia timu za madaraja ya chini kwa lengo la kuibua vipaji.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi katika uwanja  wa Maisara baada ya kumalizika mazoezi majira ya asubuhi, alisema timu hizo zikiwa na muendelezo mzuri utakuza vipaji na kuleta maendeleo.

Alisema timu za madaraja ya chini zimekuwa na uhaba wa vifaa pamoja na ukosefu wa fedha,jambo ambalo linawapa wakati mgumu katika kufikia malengo yao.

Pia alisema Serikali  imekuwa mstari wa mbele katika kuendeleza michezo kwa vijana, kwani mifano mingi inaonekana kwa kujengewa viwanja Unguja na Pemba ili kusudi kupata wachezaji wa kuitangaza Zanzibar kimichezo.

“Tunaipongeza Serikali kuinua michezo lakini sisi wa madaraja mengine tutupiwe  macho na kuungwa mkono kwa kuangaliwa changamoto zetu ili kusudi kuendeleza soka kwani vipaji huanzia ngazi za chini” alisema