NA LAYLAT KHALFAN, FATMA KITIMA

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imewataka  wananchi wanaotumia eneo la bahari pamoja na wanaoishi karibu na bahari ya Hindi, kutokuwa na hofu na kuendelea na shughuli zao kama kawaida.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mmamlaka hiyo Said Khamis Said, alitoa taarifa kwa umma kufuatia tetemeko la ardhi chini ya bahari ya hindi.

Alisema kutokana na tetemeko hilo kutokea katika eneo la chini ya bahari , mamlaka hiyo imefanya uchambuzi wa taarifa za tetemeko hilo katika kituo cheke cha tahadhari ya Tsunami ili kama kuna uwezekano wowote wa tetemeko hilo kusababisha mawimbi ya Tsunami baharini.

Aidha alieleza kuwa tetemeko hilo halikuwa na nguvu kubwa na hakuna maporomoko ya ardhi yaliyojitokeza baharini ambayo yangeweza kuzalisha tsunami.

Tetemeko hilo lilitokea Agosti 12, juzi majira ya saa 2:15 usiku ambapo mamlaka hiyo iliweza kupokea taarifa hizo zilizothibitishwa na ‘Geological Servey of Tanzania (GST), lenye ukubwa wa wa kipimo cha 5.9 katika eneo la kusini mashariki mwa Mkoa wa Pwani katika bahari hiyo.