WASHINGTON,MAREKANI

RAIS  wa Marekani Donald Trump ametia saini maagizo manne ya Rais akirefusha hatua za kutoa misaada ya kifedha kwa Wamarekani walioathirika na janga la virusi vya corona huku uchunguzi wa maoni ya wapiga kura ukionyesha idadi kubwa ya wapiga kura hawafurahi jinsi anavyolishughulikia janga hilo.

Hatua hizo nne zilionyesha uwezo wa Rais baada ya chama cha Rais huyo cha Republican na kundi la maofisa wa Ikulu ya White House kushindwa kukubaliana na upande wa upinzani bungeni wa chama cha Democratic kuhusu mpango mpya wa ufufuaji wa uchumi unaolenga kuwalinda Wamarekani wenye matatizo kutoathirika zaidi kutokana na janga hilo.

Huku idadi ya ukosefu wa ajira ukiwa juu,biashara kutatizwa kutokana na watu kutakiwa kukaa mbali mbali na kuenea kwa haraka kwa virusi vya corona, Wamarekani wengi walikuwa wakitegemea hatua za misaada zilizoidhinishwa awali na bunge ambazo nyingi zilifikia muda wake wa mwisho mnamo Julai 11.