HIVI karibuni rais wa Marekani, Donald Trump alikaririwa akitoa wito wa kutaka uchaguzi wa rais utakaofanyika nchini humo mwezi Novemba mwaka uahirishwe.

Sababu kubwa iliyotolewa na Trump ya kutaka uchaguzi huo uahirishwe ni kwamba kuongezeka kwa upigaji kura kwa njia ya posta kunaweza kusababisha udanganyifu na matokeo yasiyo sahihi.

Kuna ushahidi mdogo wa madai ya Trump, lakini kwa kipindi kirefu amekuwa akipinga upigaji kura kwa njia ya posta ambao anadai unaweza kusababisha udanganyifu.

Majimbo mengi ya Marekani mwaka huu yanataka upigaji kura ufanyike kwa njia ya posta hali ambayo itaondosha wasiwasi uliopo wa kusambaa kwa maradhi ya corona endapo watu watasongamana na kukusanyika kwneye vituo vya kupigia kura.

Katika ujumbe wake kwa njia ya Tweeter, Trump alisema kupiga kura kwa njia ya posta kutafanya uchaguzi wa Novemba kuwa usio sahihi na wenye udanganyifu mkubwa katika historia ya nchi hiyo na aibu kubwa kwa Marekani.

Alisema hivyo bila kutoa ushahidi wowote kwamba kupiga kura kwa njia ya posta kama inavyofahamika Marekani, kutahatarisha uchaguzi kuingiliwa na nchi za kigeni.

“Wanazungumza kuhusu uchaguzi kuingiliwa na nchi za kigeni, lakini wanajua kwamba upigaji kura kwa njia ya posta ni njia rahisi ya nchi za kigeni kuuingilia”, Trump alitahadharisha.

Trump aliongeza kuwa njia hiyo tayari inadhihirisha kwamba hilo litakuwa matatizo tu katika maeneo ambayo imejaribiwa.

Mapema mwezi huu, majimbo sita ya Marekani yalikuwa yanapanga kufanya uchaguzi wa mwezi Novemba kwa njia ya posta. Majimbo hayo ni pamoja na California, Utah, Hawaii, Colorado, Oregon na Washington.

Majimbo hayo yamepanga kuwa yatatuma kura moja kwa moja kwa njia ya posta kwa wapiga kura wote waliosajiliwa na baada ya hapo zitarejeshwa tena au kuwasilishwa siku ya kupiga kura, ingawa kupiga kura moja kwa moja bado kutakuwepo kwa wachache ambao hali italazimu kufanya hivyo.

Chini ya sheria ya uchaguzi wa urais, Trump hana mamlaka yoyote ya kuahirisha uchaguzi yeye binafsi na tukio kama hilo ni lazima liidhinishwe na bunge ambalo kwa kiasi fulani linaongozwa na Democrats.

Mnamo mwezi Juni mwaka huu, jimbo la New York liliruhusu wananchi kupiga kura kwa njia ya posta katika uchaguzi wa awali wa chama cha Democratic kumtafuta mgombea wa kupeperusha bendera ya chama.

Hata hivyo, changamto iliyojitokeza ni kuchelewa kuhesabiwa kwa kura hali ambayo hadi kufikia sasa matokeo bado hayajulikani.

Vyombo vya habari vimesema kwamba pia kuna wasiwasi kuwa wapiga kura wengi hawatahesabiwa kwasababu hawakujazwa vizuri au pengine hawana alama zinazoonesha kwamba kura zao zilitumwa kabla ya siku ya upigaji kura kufikia ukomo wake rasmi.

Hata hivyo kuna majimbo mengi ambayo kwa muda mrefu sasa wamekuwa yakipiga kura kwa njia ya posta na mfumo huo umeonesha mafanikio makubwa.

Rais pia anastahili kujua kwamba kwa kuandika ujumbe kwenye Twitter kuhusu uchaguzi uahirishwe au hata kama atasema “Nauliza tu!” – ana uhakika kwamba atasababisha cheche za kisiasa hasa baada ya kukataa mara kadhaa kusema ikiwa atakubali matokeo kama mambo yatamwendea mrama kwenye uchaguzi.

Trump anaonekana kufanya kila analoweza ndani ya uwezo wake kushusha uaminifu wa uchaguzi wa Novemba ambapo raia kadhaa wa Marekani inatarajiwa kwamba watategemea kupiga kura kwa njia ya posta.

Mara kadhaa amekuwa akisema madai ya uongo na yenye kupotosha kuhusu kutegemewa kwa njia ya posta na kusema kwamba kutakuwa na ulaghai kutoka mataifa ya nje.

Wakosoaji wake wameonya kwamba huenda anatengeneza mazingira ya kupinga matokeo ingawa pengine nia yake ni kuwa ni kisingizio iwapo atashindwa kwenye uchaguzi huo.

Ujumbe wa Trump wa Twitter pia unaweza kuwa dhamira yake ni kutaka kubadilisha angalizo la watu kutoka kwa takwimu za uchumi za robo ya pili ya mwaka zilizotolewa hivi karibuni.

Amekuwa akitegemea sana uchumi kupata nafasi ya kujilabu vyema kwenye kampeni zake za kuwania urais kwa awamu nyengine, lakini jinsi takwimu hizo zilivyo, mambo ni tofauti na matarajio yake.

Huku Trump akitaka kuahurishwa kwa uchaguzi kwa muda wa miezi mitatu amekuwa akipingwa dhidi ya maoni yake hayo kikiwemo hata chama chake cha Republican.

Wachumi wa Marekani wanaeleza kuwa uchumi wa nchi hiyo umeathirika vibaya ambapo hali hiyo imesababishwa ukosefu wa ajira.

Aidha wakosoaji wamesema hali hiyo imetokana na usimamizi mbaya wa janga la maambukizi ya virusi vya corona na kwamba ndio sababu kubwa kwa nini Trump anakabiliwa na kitisho cha kushindwa katika uchaguzi utakaokuwa katika muda usiozidi siku 100 zijazo.

Kura za maoni zinaonesha kwamba Trump atashindwa uchaguzi kutokana na kupoteza umaarufu wake. Trump, ambaye atapambana kwenye kinyang’anyiro hicho na mgombea wa chama cha Democrats Joe Biden ifikapo Novemba 3, hana mamlaka ya kikatiba ya kubadilisha tarehe ya kupiga kura, ambayo imeidhinishwa kisheria.

Aidha kurudia kwake mara kwa mara wazo lake la kusogezwa mbele tarehe ya uchaguzi kunakiuka desturi ya marais wa Marekani na hatua hiyo imeongeza mvutano wakati huu ambapo vyama vya kisiasa nchini Marekani vinasuguana kuhusu namna ya kukabiliana na janga la corona.

Kamati ya kitaifa ya demokrasia imesema katika taarifa yake kwamba vitisho vya Trump ni ishara kwamba amekata tamaa na hivyo anajaribu kuvuruga. Kamati hiyo imesema rais Trump anaweza kuandika kwenye Twitter yote anayotaka, lakini ukweli ni kwamba hawezi kuchelewesha uchaguzi.

Wanachama wa chama cha Republicans wanasema hawakubaliani na Trump na kwamba uchaguzi wa rais umepangwa kufanyika kisheria na wala Marekani katika historia yake haijawahi kuruhusu kucheleweshwa uchaguzi.

Wakati ambapo Baraza la Wawakilishi linadhibitiwa na chama cha Democrats na lile la Seneti linadhibitiwa na chama cha Republicans ni wazi kwamba kwa upinzani uliopo, wazo la Trump halitafika mbali.