ZANZIBAR inaelekea kwenye uchaguzi mkuu ambao kwa kawaida hufanyika kila baada ya miaka mitano na kwa mwaka huu unatarajiwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu.
Uchaguzi huo, utamuwezesha kila mwenye sifa ya kupiga kura hapa visiwani kupiga kura tano, ambapo kura tatu ni kwa ajili ya viongozi wa Zanzibar na kura mbili kwa ajili ya Jamhuri ya muungano.
Kura tatu za Zanzibar ni pamoja na kura ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, kura ya mjumbe wa baraza la wawakilishi na kura nyengine ya diwani.
Kwa upande wa serikali ya Jamhuri ya Muungano kura zitakuwa mbili ikiwemo kura ya Rais wa Jamhuri ya Muungano na kura ya mbunge ambaye atawakilishi kwenye bunge la Jamhuri.
Lakini kabla ya kuingia rasmi kwenye kampeni Tume ya Uchaguzi huandaa rasimu ama kanuni za maadili ya uchaguzi yanayobainisha mambo yepi vyama vinaruhusiwa kuyafanya na yepi vyama haviruhusiwi kuyafanya.
Bila shaka kwenye mchakato wa maandalizi ya kanuni za maadili ya uchaguzi, huvishirikisha vyama vyote vilivyothibitisha kushiriki kwenye uchaguzi na katika hili ushirikishwaji wa vyama ni muhimu kwa sababu vyama ni wadau muhimu sana.
Hatua ya Tume kuandaa kanuni za maadili ya uchaguzi una muhimu mkubwa hasa ikizingatiwa kuwa utaepusha kuwepo misigano baina ya wagombea kutoka chama kimoja na chama chengine hasa wakati wa kampeni.
Uchaguzi wa kisiasa bila ya kuekewa kanuni za maadili maana yake ni kwenda kushuhudia vurugu na hatimaye kuishia kwenye machafuko ambayo Zanzibar tusingependa tufikie huko.
Uchaguzi wa kisiasa usio na kanuni za maadili ni sawa na kandimu mpira wa kitoto unaochezwa kwenye kiwanja cha vumbi, ambapo hauna muamuzi, hauna wasaidizi waamuzi, sheria za soka hazitumiki, anayefanya faulu hapewi kadi.
Kwenye uchaguzi huwezi suala la sheria kuepuka, lazima zifuatwe kwa sababu ndizo inazotoa haki na unapokuwa na kanuni za maadili ndizo zinaobainisha kipi kifanywe na kipi kisifanywe.
Uzoefu unaonesha kuwa mara wakati wa kampeni wapo baadhi ya wagombea hujiandaa kuwatukana na kuwachafua wenzao, badala ya kutumia nafasi hiyo kueleza ilani na sera zinazobainisha nini watafanya baada ya kushinda nafasi.
Wakati mwegine mgombea anapoona hana nguvu za kushinda, hana uwezo ama hana ilani ya kueleza mbele ya wananchi huishia kushambulia, kupakazia yaliyo ndiyo na yaliyokuwa siyo, wakati mwengine hufikia hata kwenda mbali kufanya jinai.
Tuipongeze Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) na vyama vya siasa vitakavyoshirikia kwenye uchaguzi mkuu wa Zanzibar, ambavyo vimekubali kusaini kanuni za maadili ya uchaguzi.
Tunaamini kwa sababu vyama vimeshiriki kikamilifu katika maandalizi, hatuna shaka vitawalazimisha wagombea wao kuutekeleza waraka huo ambao kwa kiasi kikubwa utuepusha kuingia tusiko kutarajia.
Uchaguzi ni mchezo wa kisiasa, lakini kama wapo wagombea 100 wanaowania kiti kimoja anayehitajika ni mmoja, sio kila mgombea anaweza kuwa rais, mbunge, mwakilishi ama diwani, hivyo hakuna haja ya kuanzisha machafuko.
Yanini kuhasimiana, yanini kutukanana, yanini kuchafuana eti kwa sababu ya kisiasa wakati Wazanzibari sote ndugu wa damu. Tunavyoelewa Watumbatu, Wanungwi, Wabubwini wana ndugu Pemba na Wapemba wanandugu wa damu Makunduchi, Jambiani na Paje.
Tunachoweza kusema ni kwamba baada ya uchaguzi maisha yapo, lakini ili uchaguzi uwe wa amani lazima vyama visimamie utekelezaji wa maadili ya uchaguzi.