TUKIWA tunaisogelea Oktoba 28 ya mwaka huu, siku ambayo watanzania watashuka vituoni kwenda kufanya uamuzi wa kuchagua viongozi wapya watakaoshika nafasi kwa muda wa miaka mitano ijayo.
Mfumo wa siasa Tanzania unatoa fursa kwa vyama kusimamisha wagombea kwa nafasi zote zinazoshindaniwa na kwamba sheria bado hazijatoa fursa kwa wagombea binafsi kuingia kwenye kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya kisiasa.
Tunapenda kuchukua fursa hii kuvipongeza vyama vyetu vya siasa kwa kukamilisha zoezi gumu lililokuwa na changamoto kubwa la kusimamisha wagombea wangazi mbalimbali kuanzia urais hadi udiwani.
Vyama vyote vilipofungua milango ya uchukuaji fomu kwa ajili ya kuwania nafasi za uongozi, makada wengi sana wenye sifa walijitokeza na kutumia fursa ya kidemokrasia ya kuchagua na kuchaguliwa.
Jambo tulilojifunza ni kwamba baada ya michakato ya uchaguzi wa wagombea ndani ya vyama kukamilika kati ya watu wengi waliojitokeza kuchukua fomu mmoja ndiye aliyepitishwa na kuthibitishwa kugombea.
Hii ni fursa muhimu ya kudhihirisha kuwa nchi yetu inakomaa kisiasa na lazima tukubali nafasi nyeti zinazogombewa kwa ajili ya kufanya maamuzi ya nchi, kupitisha sera za nchi, nafasi zenye maslahi mazuri kila mmoja anaweza kuvutiwa kugombea, lakini anayeshinda ni mmoja.
Kama michakato ya vyama ilivyofanikiwa ya kupata mgombea mmoja kati ya wagombea zaidi ya 20, tungependa kuona wagombea kutoka vyama mbalimbali pia wanakubaliana na matokeo baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 28 mwaka huu.
Wakati tunakwenda kwenye uchaguzi mkuu, ni vizuri sana kila mgombea kutoka kila chama cha siasa na kila mdau wa uchaguzi akahakikisha kwamba anafanya lile lililokwenye mipaka yake ya sheria.
Lazima tukumbuke kuwa pale mipaka yako inapoishia ndipo jukumu la mtu mwengine linapoanzia, hivyo kuingia kwenye jukumu la mwengine ni kusabisha uvunjaji wa sheria na wakati mwengine ni uhalifu.
Kwa mfano tumeanza kusikia baadhi ya wanasiasa wanajenga misimamo hasi na kuhamasishana kusikokuwa na hatuma njema kwa amani ya nchi kwa kusema kuwa lazima walinde kura zao, lazima wasimamie kura zao?
Hebu tuwaulize hao wanaohamasishwa na kushajihishwa kulinda kura ni vyema nao wao wenye wakajiuliza, mamlaka hayo ya kulinda na kusimamia kura zao baada ya kupigwa unayapata wapi?
Ni vyema pia wakajiridhisha kwa kuisoma sheria inasemaje baada ya zoezi la kura kukamilika? Na je hivi unafikiri huyo mwenye mamlaka ya kulinda kura anaweza kukupa nafasi isiyoyako ya kulinda kura?
Tunatahadharisha kwa kuwaeleza wafuasi wa kisiasa ambao wanafuata mikumbo na mihemko kwamba, kabla ya kuhamasika kutekeleza agizo la chama au la mabosi wa chama la kulinda kura, isome sheria inasemaje isijekuwa wanakuchimbia shimo.
Umefika wakati tuaminiane na kwamba wazanzibari ni ndugu na tusitenganishwe na michakato ya kisiasa, hasa ikizingatiwa kuwa yapo maisha marefu baada ya siku moja tu ya uchaguzi.