ZASPOTI

MCHEZO wa soka ni mmoja wa michezo maarufu duniani kote ambao una mashabiki wengi wa jinsia zote na rika tofauti.

Takriban duniani kote mchezo huo umejizolea sifa na kuwa mchezo wa kwanza wenye mashabiki wengi.

Nchi mbali mbali duniani wachezaji wa soka huzitangaza vyema nchi zao, pamoja na kuwa na kipato kikubwa.

Nchi mbali mbali duniani huwafunza vijana wao wadogo ambao wanapendelea mchezo wa soka na kufanikiwa kwa kupata wachezaji wazuri.

Lakini mbali na hilo pia huanzisha timu za watoto wadogo ambapo baaade wachezaji hao hutegemewa baada ya kulelewa na kufunzwa mambo mengi.

Kwa hapa nyumbani Zanzibar tumeona zipo timu nyingi za watoto wenye umri mdogo ambazo hujikusanya kwa pamoja na kucheza ligi.

Katika miaka ya karibuni tumeshuhudia mlinda mlango wa zamani visiwani humu, ambae aliwika katika timu mbali mbali zikiwemo za taifa Ali Bushuri akianzisha akademi  ya watoto.

Kuanzisha kwa akademi hiyo inayojuliakana kwa jina la Kituo cha Kukuza na Kulea Vipaji(YFDA), ni faraja kubwa sana, kwani itaweza kusaidia soka la Zanzibar kupatikana wachezaji wenye viwango na ujuzi wa hali ya juu.

Lakini mbali na mchezo wa soka na sheria zake, Ali Bushiri huwalea watoto hao  kwa kuwapa mafunzo mbali mbali, ikiwemo  kuwazungumzisha lugha ya Kiingereza,maadili mema,usafi pamoja na heshima uwanjani na mitaani.

Hivi sasa soka ni ajira, kwa maana hiyo kitendo cha Bushiri kutumia lugha ya Kiingereza kuwafunza vijana hao ni sahihi , kwani itasaidia mchezaji kuelewa mambo mbali mbali.

Njia anazozitumia mwanasoka huyo wa zamani ni za kuigwa na kupigiwa mfano, kwani nchi yetu tunaweza kusema yeye ni mtu wa kwanza kufanya jambo hili ambalo ni zuri kwa taifa zima.

Tukubali tukatae lakini jukumu analolibeba mwalimu huyo kwa kuwakusanya watoto wengi na kuwapa  mafunzo stahiki ambayo yatawasaidia hapo baadae zithaminiwe.

Tufahamu kwamba kazi ya kulea mtoto ni kubwa na inahitaji ustahamilivu,tumeshuhudia wazazi mbali mbali wakielezea ugumu wa malezi ya watoto wao.

Hayo anayoyafanya Bushuri hakutumwa na mtu bali ni mapenzi makubwa aliyonayo kwa taifa lake,hivyo ni vyema kumuunga mkono na kuthamini mchango wake kukuza vipaji vya vijana wa Kizanzibari.

Nimegundua kwamba lengo lake ni kuona Zanzibar nayo imo katika ramani ya dunia yenye wachezaji wazuri na wenye maadili ya heshima kupitia tamaduni za Kizanzibari.

Imani yangu kubwa kwa mkufunzi huyo kwamba baada ya miaka mitano mpaka saba,Zanzibar tutakuwa na vipaji vingi vya mchezo wa soka na hata kununuliwa katika nchi mbali mbali duniani.

Wazanzibari hatuna budi kumuunga mkono mkufunzi huyo ambae amejitolea kuhakikisha soka la Zanzibar linarudi hadhi yake kwa kutumia utaratibu wa kisasa.

Hili sio jambo geni duniani kwani nchi mbali mbali zimefanikiwa kutokana na kuanzisha akademia za kukuza vipaji kwa vijana wadogo katika mataifa yao.

Hivyo kuthamini juhudi na bidii zinazochukuliwa na mwalimu huyo mzalendo naamini zitasaidia kuinua soka la nyumbani na kupata mafanikio makubwa kama wanayoyapata wenzetu nchi mbali mbali duniani.