NA MADINA ISSA

KAIMU Msimamizi wa Uchaguzi wilaya ya Mjini, Haji Hassan Khamis, amewataka wagombea wanaokwenda ofisini hapo kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa na Tume, kuwa makini wakati za kuzijaza ili kuepuka usumbufu.

Akizungumza na waandishi wa habari, mara baada ya kumkabidhi mgombea fomu za kuomba kuteuliwa nafasi ya ubunge jimbo la Kikwajuni kupitia CHADEMA, huko Maisara alisema ni vyema wagombea wakazingatia maelezo yaliyomo kwenye fomu hizo.

Alisema endapo waomba nafasi za uongozi kutoka vyama mbalimbali vya siasa wanaoomba uteuzi watazijaza fomu hizo vizuri wataepuka usumbufu wa kurejeshwa kuzijaza tena kama zitabainika kuwa na makosa.

Alisema Tume inawashauri waomba nafasi za uongozi wanapochukua fomu kuzirejesha siku tatu kabla ya zoezi hilo kufungwa ili kuepusha changamoto zinazoweza kujitokeza.

“Tunajua binaadamu anaweza kukosea hivyo kurejesha mapema kunasaidia kukaguliwa vizuri na endapo tukibaini kuwa zina mapungufu tunaweza kumrejeshea kwa ajili ya marekebisho, sio vyema kusubiri siku ya mwisho”,alisema.

Alisema kuwa zoezi hilo limeanza Agosti 12 na linaendelea vizuri na hakuna tatizo lolote lililojitokeza waomba nafasi za uongozi kutoka vyama mbalimbali wanaendelea kujitokeza kuchukua fomu.

“Bado mapema siwezi kutaja vyama vilivyokuwa vishajitokeza kuchukua fomu ila zoezi linakwenda vizuri kama lilivyopangwa”, alisema.

Sambamba na hayo, alifahamisha kuwa endapo mgombea nafasi ya ubunge atapata asilimia 10 za kura zake jimboni atarejeshewa fedha zake alizozitoa katika uchukuaji wa fomu hiyo.

Hapo juzi wagombea waliojitokeza kuchukua fomu hiyo ni wa chama cha CHADEMA ambapo mgombea wa nafasi ya ubunge jimbo la Kikwajuni, Zeyudi Mvano Abdullah na Mgombea wa nafasi ya Ubunge jimbo la Pangawe, Hudhaima Ali Hamdani walijitokeza na kuchukua fomu.