ZANZIBAR ni nchi yenye historia kubwa na vivutio vingi vya kitalii ambavyo vimekuwa vikiingizia fedha nyingi za kigeni na hivyo kuinua uchumi wake na hali za wananchi kwa jumla.

Miongoni mwa vivutio hivyo, ni urithi wa Mji Mkongwe, magofu ya kihistoria yaliyoenea kila pembe Unguja na Pemba, fukwe za kuvutia, mashamba ya viungo, na zaidi akhlaki za watu wake ambao wanasifika kwa ukarimu na tamaduni zao.

Lakini pamoja na sifa zote nzuri ambazo Zanzibar inazo, bado tatizo la uchafu wa mji ni jambo linalotia doa taswira hiyo njema kwa nchi yetu.

Na hili ndilo linalosababisha mripuko wa maradhi mbalimbali ikiwemo kipindupindu ambacho mara kadhaa kimekuwa kikileta athari kubwa huku serikali ikilazimika kupiga marufuku baadhi ya biashara za vyakula na karamu.

Pamoja na elimu yote inayotolewa kila siku na mamlaka zinazohusika na maendeleo ya miji juu ya umuhimu wa kuiweka safi, bado miji na mitaa yetu iko katika hali ya uchafu unaoiweka nchi katika ramani mbaya.

Licha ya jitihada za mabaraza ya manispaa, bado mitaa yetu mijini na ng’ambo inatia jelezi kuiona kwani taka zinaachwa zikizagaa barabarani na vichochoroni na kuzalisha nzi ambao ni hatari kwa afya za wakaazi na wageni wafikao hapa.

Lililo baya na la aibu zaidi, ni kwamba sisi ni binadamu ambao kimsingi tunatakiwa tufahamu maana na umuhimu wa usafi na tusiwe watu wa kufundishwa na kuhimizwa tu juu ya jambo hilo.

Hatuoni mantiki ya watu wazima kuwa kila siku wanakumbushwa kuweka mazingira safi, lakini Rais wetu Dk. Ali Mohamed Shein ahajachoka kutuhimiza kuhusu usafi.

Usafi ni jambo ambalo mtu mwenye akili timamu na maarifa ya kiutu uzima, anapaswa kulifahamu na kulifanya kuwa sehemu ya utamaduni wa maisha yake ya kila siku.

Hivi kweli watu wazima ambao wanajua madhara ya uchafu katika baadhi ya mitaa na maeneo mbalimbali ya miji yetu kuwekwa mabango yanayoandikwa matangazo ya kukataza watu kutupa taka, au kwenda haja ndogo?

Kwa nini mtu mzima na akili zako, utoke nyumbani kwako na kipolo cha taka na kwenda kuzitupa kwenye mtaro wa maji machafu, pembezoni mwa nyumba ya mtu mwengine, au wewe unaeishi ghorofani huoni vibaya kurusha taka, ‘pampers’, au maji machafu kutoka juu kwa kupitia varanda?

Tunapofanya mambo mengine, lazima tupime athari zake, na pia tujiulize iwapo mtu mwengine atatufanyia sisi tutafurahi?

Ni vyema katika hali ya kawaida, wazazi tunapaswa kuwafundisha watoto wetu umuhimu wa usafi, lakini kinyume chake, sisi tumekuwa watu wa kufundishwa na mabaraza ya miji, kwani ndio wachafuzi wakubwa wa mazingira tukiwa nje ya nyumba zetu.