TUNAZIPONGEZA jitihada kubwa za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuwapa matibabu bure wananchi wake kutokana na kusumbuliwa na magonjwa kadhaa ikiwemo yale yasio ya kuambukiza na yanayoambukiza.

Katika maisha ya kisasa wananchi wengi wa Zanzibar afya zao zimekuwa zikizorota kutokana na ongezeko kubwa la maradhi yasio ya kuambukiza.

Hivi sasa Zanzibar imekuwa na idadi kubwa ya wagonjwa wanaosumbuliwa na maradhi ya shinikizo la damu, saratani za aina mbalimbali na kisukari, magonjwa ambayo yamechukua nafasi kubwa na kusababisha watu akdhaa kupoteza maisha.

Si jambo la kushangaza kumuona kijana mbichi wa miaka 20 akisumbuliwa na maradhi ya sukari na shindikizo la damu wakati katika miaka ya nyuma maradhi haya yalikuwa ya watu wenye umri mkubwa.

Aidha maradhi hayo pia yalikuwa ya watu walionekana kuwa wanamaisha mazuri na si aghalabu maradhi hayo kuwakuta wananchi masikini, lakini sasa hivi hata masikini nao yanawakumba.

Jamii lazima ielewe kuwa maradhi yasiyoambukiza kikiwemo kisukari, shindikizo la damu na saratani za aina mbalimbali ni maradhi yanayotesa kutokana na maumivu makali, huku pia kwa wagonjwa wa kisukari wakipoteza hata sehemu za miili yao.

Katika familia zetu tunao watu ambao wanaugua maradhi hayo, wapo ambao wameshapoteza viungo na wengine wanaendelea na matibabu katika hospitali zetu za Unguja na Pemba kutokana na maradhi yasiyoambukiza.

Kiukweli magonjwa hayo yanatishia maisha ya wazanzibari na endapo watalamu hawatashiriki kuisaidia jamii katika kuipa taaluma za kuepukana nayo ugonjwa huo, hali inaweza kuwa mbaya sana.

Tunasema elimu ya afya dhidi ya maradhi yasiyoambukiza inahitajika katika jamii kwani wapo baadhi ya wananchi wanaopata maradhi hayo wanakimbilia kwa waganga wa kienyeji kutafuta tiba.

Kwa bahati mbaya sana kila wakikimbilia huko ndipo mambo yanapokuwa magumu zaidi kwani hakuna ahuweni wanayoipata badala ya kuongeza maradhi zaidi.