MIAKA 10 ya serikali ya awamu ya saba inaelekea ukingoni, kwa hakika tutaikumbuka serikali hii inayoongozwa na Dk. Ali Mohamed Shein kwa hatua kubwa za kimaendeleo zilizofikiwa.

Hakuna eneo la kiuchumi na kijamii ambalo katika miaka 10 ya serikali ya awamu ya saba inayomaliza muda yake haikutia mkono wa kuchapuza maendeleo.

Tunajua lipo kundi la watu lilianza kubeza tangu siku ya kwanza Dk. Shein anaingia madarakani, lakini kadiri alivyo dhihirisha vitendo vyake wengine waliungama na kuungana naye.

Lakini pia wapo walioendelea kujitia upovu ingawaje wana macho na wapo waliojitia uziwi ingawaje wana masikio mawili na wanausikivu wa kutosha, ambao mapaka leo wanaendelea na mabezo yao.

Hata hivyo wakati serikali ya awamu ya saba inaondoka madarakani na kuipisha serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya awamu ya nane ianze kushina nafasi yake lazima tuwe makini sana.

Uzoefu unaonesha kuwa muda wa kubadilisha awamu unapowadia, baadhi ya watumishi wasio waamini hukitumia vibaya kipindi hicho kuihujumu serikali inayoondoka na kuichafulia sifa na heshima yake.

Tunachotaka kusema uzoefu unaonesha kwamba baadhi ya watumishi na watendaji hukitumia kipindi hicho kujinufaisha kwa kujimilikisha baadhi ya mali za serikali na wengine hufikia hatua kuhujumu.

Huu ndio wakati kwa baadhi ya watendaji kujimilikisha mali mbalimbali za serikali ikiwemo gari, ambazo zimewekwa pembeni ya jengo la ofisi zikiwa hazitembei lakini nzima.

Wakati ndio mambo mbalimbali yasiyopendeza ikiwemo hata kufunjwa kwa fedha za serikali, mambo ambayo ni kinyume na sheria za utumishishi wa umma.

Yote yanayofanyika lengo lake ni kiudhoofisha serikali kuiondolea hadhi na heshima yake hasa ikizingatiwa kuwa ilisimamia majukumu yake vyema.

Ushauri wetu ni kwamba huu ni wakati wa serikali kuhakikisha inadhiti upotevu wa mali zake na kuziba nyufa na mivujo ya fedha za umma katika kipindi hichi ambapo tunaamini wapo waliojipanga kutekeleza maovu.