NA ABOUD MAHMOUD
BALOZI wa heshima wa Brazil Zanzibar Abdulsamad Abdulrahim, amesema ofisi yake imedhamiria kuhakikisha inakuza na kuendeleza michezo ya Soka na mpira wa Kikapu visiwani Zanzibar.
Akizungumza na Zanzibar Leo huko ofisini kwake Kiwajuni mjini Unguja,balozi huyo alisema dhamira hiyo itasaidia kuinua sekta ya michezo, ili wachezaji wake kutambulika katika nchi mbali mbali duniani.
Alisema tayari ofisi yake imekaa na kufanya mazungumzo na nchi mbali mbali, ziweze kusaidia kuinua michezo hiyo ambayo ni miongoni mwa michezo inayopendwa duniani.
Alitaja nchi ambazo zitatoa wataalamu kuja kufundisha michezo hiyo ni pamoja na umoja wa wachezaji wa soka kutoka nchini Brazil na Uingereza, na kwa upande wa mchezo wa mpira wa Kikapu tayari umezungumza na wachezaji na wakufunzi kutoka jimbo la Chicago nchini Marekani.
Alisema wataalamu hao kutoka nchi hizo tofauti walitarajiwa kufika nchini mapema mwaka huu, lakini mara baada ya kuzuka maradhi ya homa kali ya mapafu yanayotokana na virusi vya Corona iliwalazimu wasitishe ujio wao huo.
“Dhamira yetu ni kuwaleta wataalamu na wachezaji maarufu ili kutoa elimu ya michezo kwa vijana wetu, wajue nini umuhimu wa michezo na sababu zilizowafanya wenzao wakafika mbali ili na wao waweze kufanikiwa,”alisema.
Balozi huyo alieleza baada ya kupungua kwa ugonjwa huo wanatarajia wataalamu na wakufunzi hao, watafika viziwani humu kwa lengo la kufundisha mbinu za mchezo, pamoja na kuwaweka vijana wa Zanzibar katika ushindani wa kimataifa kupitia michezo hiyo.
“Tayari wachezaji wa maarufu kutoka Brazil waje akiwemo Kaka, Ronaldinho, Neymar,Roberto Carlos na wengine wengi, lakini maradhi yamewazuia ila mpango wao wa kuja bado upo na watakapokuja naamini utasaidia wachezaji wetu, kupata uelewa na kuhamasisha Zanzibar iwe nambari moja katika Afrika Mashariki kupitia Soka na Kikapu,”alifafanua.
Balozi huyo wa heshima alisema ofisi yake hivi sasa tayari wameanza kutafuta changamoto mbali mbali zinazokabili michezo hiyo ikiwemo fedha za kushiriki katika mashindano mbali mbali pamoja na viwanja vya kisasa .
Alifahamisha kwa upande wa ukosefu wa fedha wamegundua timu nyingi za kiraia hushindwa kushiriki katika mashindano mbali mbali na kuziacha zishiriki za kiaskari.
Kuhusu viwanja hasa vya mchezo wa Kikapu, Abdulsamad alisema wachezaji wengi wa Zanzibar, wanashindwa kufanya uzuri au kushiriki katika mashindano ya kimataifa kutokana na kutozoea kutumia viwanja hivyo.
Hivyo alisema alisema Ubalozi upo karibu kushirikiana na Zanzibar katika sekta mbali mbali ikiwemo ya michezo, ili vijana waweze kupata manufaa pamoja na kuitangaza vyema nchi kitaifa na kimataifa .