PARIS,UFARANSA
RAIS wa Ufaransa Emmanuel Macron ametangaza kwamba nchi hiyo itaimarisha uwepo wake wa kijeshi,katika eneo la mashariki mwa bahari ya Mediterania.
Pia aliiomba Uturuki kusitisha utafutaji wa mafuta na gesi katika eneo la maji linalogombaniwa na kuibua wasiwasi na Ugiriki.
Kwenye mazungumzo ya simu na Waziri mkuu wa Ugiriki, Kyriakos Mitsotakis, Macron alielezea wasiwasi wake kuhusiana na hatua hiyo ya upande mmoja ya utafutaji wa mafuta inayofanywa na Uturuki na kuongeza kuwa wanatakiwa kusitisha ili kuruhusu majadiliano ya amani kati yao na Ugiriki.
Kumeongezeka hali ya wasiwasi kati ya mataifa hayo mawili wanachama wa jumuiya ya kujihami ya NATO, kuhusiana na madai ya kuwepo kwa hifadhi ya gesi asilia kwenye eneo hilo.