KAMPALA,UGANDA

WIZARA  ya afya Uganda imeripoti kifo cha tano cha Covid-19 cha mwanamke mwenye umri wa miaka 46 anaeishi Kibuli akiwa na asili ya India.

Kifo hicho kinafikisha asilimia 80 ya vifo vinavyokana na Covid-19 nchini vilivyokea katika jiji la Kampala pekee.

Wataalam wanadai kuwa kuongezeka kwa vifo hivyo katika jiji hilo vinatokana na ukiukwaji mkubwa wa hatua za kuzuia Covid-19,ambapo inadaiwa kuwa vifo zaidi vikitokea Kampala bado itakuwa na sehemu kubwa zaidi ya vifo.

“Baada ya mgonjwa huyo kugundulika kuwa na Covid-19, timu ya hospitali ilimpeleka mgonjwa hospitali ya Mulago kwa usimamizi zaidi siku hiyo hiyo.Kwa bahati mbaya, alifariki wakati anakwenda hospitali ya Mulago,” ilieleza taarifa ya Wizara ya afya.

Vifo vyengine vitatu viliripotiwa ikiwa kutoka  Nakulabye kimoja, na vifo viwili kutoka Kisenyi maeneo yote yakiwa ndani ya jiji la Kampala.

Taarifa hizo zinakuja wakati nchi ina jumla ya kesi 1,195 pamoja na sampuli 280,747 zinazofanyiwa vipimo kwa sasa.

Mtaalamu wa afya ya umma katika Chuo Kikuu cha Makerere Prof Freddie alisema maambukizi ya Covid-19 na vifo vinatokea sana maeneo ya mjini kutokana  na ongezeko la watu.