ATHENS,UGIRIKI
UGIRIKI imetoa wito wa mkutano wa kijeshi baada ya Uturuki kurejesha shughuli zake za kutafuta hifadhi ya gesi karibu na kisiwa cha Ugiriki.
Wakati hayo yakijiri Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan naye alitoa wito wa mazungumzo ya kusaka suluhu ya masuala yanayoendelea kujitokeza baina ya mataifa hayo mawili wanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO.
Ugiriki iliituhumu Uturuki kwa kutishia amani katika eneo la mashariki ya Mediterania baada ya Serikali ya mjini Ankara kurejesha shughuli zake za kutafuta mafuta na gesi karibu na kisiwa cha Kastellorizo.
Ofisi ya Waziri mkuu wa Ugiriki, Kyriakos Mitsotakis ilisema imezungumza na Rais wa baraza la Ulaya Charles Michel na katibu mkuu wa jumuiya ya kujihami ya NATO, Jens Stoltenberg, aliyetoa wito wa sheria za kimataifa kuheshimiwa.
Rais Erdogan alitoa wito wa pande hizo kutafuta suluhu ya pamoja itakayolinda haki zao zote.