NA MWAJUMA JUMA

TIMU ya soka ya Muembeladu ‘kubwa lijalo’ imeendeleza uteja kwa timu ya  Ujamaa kwa kufungwa bao 1-0, katika mchezo wa ligi daraja la pili Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja uliochezwa juzi.

Mwembeladu ambayo historia inaonesha kuwa haijawahi kuifunga Ujamaa tokea zikutane katika madaraja yote ya ligi,  katika mzunguruko wa kwanza ligi hiyo walitoka bila ya kufungana.

Katika mchezo huo miamba hiyo ilionekana kukamiana na kufanikiwa kwenda mapumziko wakiwa hakuna ambae aliweza kuuona mlango wa mwenziwe.

Ujamaa ambayo ilijigamba sana baada ya kuibuka na ushindi huo ilionekana kupanga mashambulizi zaidi, katika kipindi cha pili ambacho ndicho walichoweza kupata matokeo hayo na kuondoka na pointi tatu.

Bao hilo pekee lilifungwa na  Ali Climent Maziku ikiwa zimebakia dakika 10 tu kabla ya kumalizika kwa mchezo huo.