NA ASYA HASSAN

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya biashara na Viwanda, imeanza matengenezo ya ujenzi katika eneo lililotengwa kwa ajili ya kufanyika tamasha la Mapinduzi liliopo huko Nyamanzi wilaya ya Magharibi ‘B’ Unguja.

Akizungumza na gazeti hili, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Juma Hassan Reli, alisema hadi sasa wameanza matengenezo hayo kwa kusafisha eneo hilo, pamoja na kufikisha miundombinu muhimu ya huduma za kijamii ikiwemo maji na umeme.

Alisema kukamilika kwa hatua hiyo, hatua inayofuata ni kumwaga zege katika eneo linalotarajiwa kuwekwa mabanda ya maonesho, jambo ambalo halijafanyika kutokana na uhaba wa fedha.

Akizungumzia tamasha la saba la mapinduzi kufanyika katika viwanja hivyo, Katibu huyo alisema kwa sasa mapema kuzungumzia suala hilo hadi pale taratibu za ujenzi katika eneo hilo zitapokamilika.

“Zikipatikana fedha kwa kipindi cha miezi mitatu kutamwagwa zege na kufanyika kwa matengenezo mengine muhimu na muda ukifika kutawekwa mabanda na tamasha la saba litafikyika katika eneo hilo,”alisema.

Hata hivyo alifahamisha kwamba serikali imetenga eneo la Nyamanzi kwa ajili ya kufanyika tamasha hilo kutokana na mwamko mkubwa wa watu kutoka maeneo mbalimbali kushiriki katika tamasha hilo kila mwaka, kwa kuuza na kutoa huduma nyengine, baada ya kubainika eneo la Maisara dogo na halikidhi mahitaji ya tamasha hilo.