NA MARYAM SALUM
UJENZI wa kiwanda cha kusindika mwani Chamanangwe Wilaya ya Wete, utasaidia kupunguza tatizo la ajira kwa wanawake na wavijana nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Kilimo, Mifugo, Maliasili na Uvuvi, Mmanga Mjengo Mjawiri , wakati akizungungumza na wakulima  wa mwani pamoja na viongozi wa shehia baada ya kuwakabidhi vihori vya kuchukulia mwani kutoka baharini hadi nchi kavu.
Alisema serikali iko kwenye mchakato wa kujenga kiwanda hicho ili kuhakikisha mwani unaosafirishwa unaongezewa thamani.

“Kiwanda kitakachojengwa ni kwa ajili ya kusarifia zao la mwani, ili kilimo hicho kiwe na tija zaidi,” alisema.

Aidha alifahamisha kuwa ,licha ya serikali kuwa na mpango wa kujenga kiwanda hicho,pia ipo njiani kuleta meli nne kubwa za uvuvi wa baharini kuu kwa lengo la kuwapatia wananchi wake maendeleo zaidi.

Alisema kuwa kiwanda hicho kitakua na mashine kubwa ya kuzalisha chakula cha kuku ambapo kwa siku kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 50 ambapo bei ya chakula cha kuku kitashuka.

Alisema Zanzibar ni miongoni mwa nchi zinazosafirisha mwani kwa wingi duniani, lakini mwani unaozalisha ni ghafi.