WASHINGTON,MAREKANI

MAKAMU  wa Kwanza wa Rais wa Jamuhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, ukatili wa polisi ya Marekani unatokana na chuki ya kihistoria yenye mizizi katika fikra ya ubaguzi wa rangi inayotawala nchi hiyo.

Is’haq Jahangiri alisema hayo baada ya kuoneshwa picha ya mauaji yaliyofanywa na polisi wa Marekani dhidi ya raia mweusi wa nchi hiyo katika jimbo la Arizona.

Alisema ukatili na fikra za ubaguzi wa rangi zimedhihirika vyema zaidi katika kipindi cha utawala wa Donald Trump. 

Jahangiri alikosoa vigezo  vinavyotawala dunia kuhusiana na suala la kukabiliana na uhalifu na kusema dhati ya binadamu kote duniani inalaani ukatili huo.

Vyombo vya habari vilionesha picha za mauaji ya kikatili yaliyofanywa na polisi wa Marekani dhidi ya Ramon Timothy Lopez, 28, katika jimbo la Arizona.

Katika mauaji hayo yaliyofanyika tarehe 4 mwezi huu wa Agosti, maofisa wa polisi walionekana wakimgandamiza shingoni na mgongoni kijana Timothy Lopez kwa muda wa dakika sita. Kijana huyo alipoteza fahamu na baadaye kufariki duniani.

Katika tukio jengine linalodhihirisha ukatili wa polisi ya Marekani, polisi wawili wa nchi hiyo katika jimbo la Wisconsin walimpiga risasi kadhaa raia mweusi wa nchi hiyo alipokuwa akipanda gari kwa sababu isiyojulikana.

Jacob Blake alilazwa Hospitalini kutokana na majeraha ya risasi, na baba yake anasema amepooza viungo vya mwili.

Tukio hilo limesababisha maandamano ya siku kadhaa katika mji wa Kenosha ambako wananchi wamechoma moto magari na maeneo ya umma wakipinga ukatili wa polisi ya Marekani.