NA HAFSA GOLO

MAMLAKA ya Maji Zanzibar (ZAWA) imeanza rasmin huduma ya ulipaji wa maji safi na salama kupitia mtandao wa Ezy pesa Agosti sita mwezi huu.

Ofisa Uhusiano wa Mamlaka hiyo, Amina  Abdallah Daud, alieleza hayo alipokua akizungumza na gazeti hili ofisini kwake Mabluu Unguja.

Alisema lengo la uanzishaji wa huduma hiyo ni kuharakisha ulipaji maji kwa wakati na kuepukana na ulimbikizaji wa madeni unaolalamikiwa na wateja.

Aidha alisema, huduma hiyo italeta unafuu wa kupunguza masafa kwa wateja mbali mbali wa mjini na vijijini.

Amina alisema, Mamlaka inatoa wito kwa wateja kutumia mfumo huo ambao utasaidia kurahisisha ukusanyaji wa mapato kwa wakati uliopangwa sambamba na kuimarisha huduma na miundombinu ya maji nchini.

“Mteja apige namba hii “150*02# baadae unachagua namba tano kwa ajili ya maelekezo zaidi aidha wateja wanaohitaji ufafanuzi naomba wasisite kuwasiliana na mamlaka yetu”,alisema.

Alisema kabla ya kuanzishwa kutumika utaratibu huo ZAWA ilikuwa na uwezo wa kukusanya takriban asilimia 50 ya malipo ya maji safi na salama kwa mwezi.

Alifahamisha miongoni mwa wadaiwa wakubwa ni wateja wa majumbani na taasisi za serikali pamoja na elimu inayoendelea kutolewa kuhusu umuhimu wa kuchangia huduma hiyo.

Katika hatua nyengine alisema, ZAWA mara baada ya kukamilisha zoezi la utiaji saini mradi wa maji kupitia mkopo kutoka Serikali ya India wakandarasi tayari wameshawasili nchini na wameshakabidhiwa maeneo ya ujenzi wa miundombinu ya maji.

Alitaja miongoni mwa maeneo hayo ni pamoja na Mkoa wa Mjini, Mgharibi na Wilaya ya Kati.

Mapema  gazetI hili lilifanya mahojiano na baadhi ya wananchi wanaotumia huduma ya maji safi na salama ,walisema kuanzishwa kwa malipo njia ya mtandao italeta wepesi na kupunguza gharama za usafiri.

Hafidh Juma Said alisema, zawa imefanya jambo la msingi litakaloleta unafuu kwa wateja hasa ikizingatiwa kukua kwa teknolojia nchini.

“Tunaamini mfumo uliotumiwa hivi sasa utasaidia kuongezeka kwa makusanyo iwapo watahasisha ipasavyo”,alisema.

Khadija Zakari Daud alisema, elimu ya ziada inahitajika ili watumiaji wa huduma hiyo wawe na mwamko endelevu na kuleta tija.