ZASPOTI

KWA wiki kadhaa sasa, kumekuwa na malumbano ya kiuongozi ndani ya Shirikisho la Soka la Zanzibar (ZFF), hali ambayo imekuwa ikiwachanganya wanamichezo na wananchi kwa ujumla ndani ya chombo hicho cha kitaifa.


Tofauti ya mitazamo kati ya rais wa chama hicho, Seif Kombo Pandu na Kamati ya Utendaji ya ZFF, imesababisha malumbano yasiyokuwa ya lazima baina ya pande hizo zenye jukumu la ustawi wa soka visiwani hapa.


Tungelipenda kuchukuwa nafasi hii kuzitaka pande hizo kukaa pamoja na kumaliza tofauti zao ili kuepusha mgogoro unaowezakujitokeza nndani ya chombo hicho.
Ni ukweli uliowazi kwamba migogoro mingi inajitokeza ndani ya vyama vya michezo hutokana na kutofuatwa kwa katiba zao ambazo tayari zimesajiliwa kwa muda mrefu na Mrajis wa Vyama na Klabu.


Zanzibar ni nchi inayojipambanua kwamba ni ya wapenda michezo kutokana na jinsi wananchi wake walivyo na hamasa na ushabiki wa michezo mbalimbali bila ya kuwepo ushawishi wowote.
Kwa mantiki hiyo, ushabiki na mapenzi ya michezo kwa wananchi yapo dhahiri kama ilivyo kwa mataifa mengine ambayo michezo imejengewa misingi bora na yenye kuleta tija badala ya malumbano.


Ni ukweli usiopingika kwamba Zanzibar imejaaliwa kuwa na wanamichezo wenye vipaji na wanaoweza kucheza popote, lakini, kinachokosekana ni usimamizi kwa baadhi ya viongozi waliopewa dhmana jambo ambalo hivi sasa linahitaji kufanyiwa marekebisho makubwa ili kupata viongozi watakaokuwa tayari kwa hilo.


Tunasema hivyo kutokana na yale ambayo yamekuwa yakiendelea kwenye vyama vyetu vya michezo kwa kuwepo tofauti za kimakundi ndani ya safu za uongozi, hali ambayo imekuwa ikitajwa kurudisha nyuma maendeleo ya michezo kwa miaka mingi.


Lakini, tukiwa wadau wakubwa wa michezo, tunaamini ikiwa kasoro kama hizo zitafanyiwa kazi kikweli, tunaweza kutoa sura mpya ya michezo Zanzibar na kuwa chachu ya kujikwamua hapa tulipokwama sasa kutokana na sababu mbalimbali.


Ni dhahiri kwamba tumekuwa na kiu kubwa ya kupata mafanikio ya michezo sambamba na kuziona timu zetu zikicheza hatua ya juu zaidi ya michuano mbalimbali ya kimataifa kwa mustakabali wa nchi na maendeleo yake kwa ujumla.


Kutokana na hali ilivyo ni wazi kwamba tunahitaji kujipanga upya tukiwa na mtazamo tofauti na mipango madhubuti ya kurudisha heshima ya michezo katika visiwa hivi.
Lakini ukweli unabakia pale pale kwamba tunahitaji kwenda mbali zaidi huku tukiwa na ujasiri wa kuamini kwamba tunaweza kuvuka kutoka hatua moja na kusogea mbele zaidi ikiwa kila mmoja wetu atatimiza wajibu wake.


Kinachohitajika hapa kwanza ni kujitathimni na hali tunayoendelea kuizoea ya kuwa watu tuliokosa mipango na kufanya mambo kwa mazoea bila ya kujali gharama ambazo viongozi wetu wa juu wa nchi wanaingia katika kuinua sekta ya michezo kama zilivyo kwa sekta nyengine.
Hatukusudii kumnyooshea kidole yoyote yule, bali ni kuangalia njia za kujitathimni na kuelewa wapi tunakoelekea ikiwa hali ya sasa ya michezo yetu itaendelea hivi ilivyo sasa.


Hivyo, lazima tufike mahali na kuondokana na migogoro ndani ya vyama vyetu huku tukihitaji maendeleo chanya ya michezo kwa ajili ya taifa.
Zanzibar yenye maendeleo ya michezo inawezekana.