UTAFITI wa kimataifa wa unyonyeshaji uliongonzwa na Shirika la Afya duniani (WHO) unaonesha kuwa hakuna nchi inayokidhi kikamilifu viwango vya unyonyeshaji vinavyopendekezwa kitaalamu.
Viwango vya unyonyeshaji vilivyofanyiwa tathimini katika nchi 194 vimebaini kwamba ni asilimi 40 tu ya watoto walio chini ya umri wa miezi sita wananyonyeshwa maziwa ya mama pekee bila kitu kingine na nchi 23 pekee duniani ndizo zenye kiwango cha unyonyeshaji pekee wa zaidi ya asimilia 60. Inasikitisha.
Kwani kwa miezi 6 ya mwanzo, maziwa ya mama yana virutubishi vyote kwa uwiano sahihi, pamoja na maji, vinavyohitajika kwa ukuaji wa mtoto kiakili na kimwili.
Maziwa ya mama ya mwanzo yana kinga mwili zenye uwezo mkubwa wa kumkinga mtoto dhidi ya magonjwa mbalimbali ambayo yanayoweza kuathiri ukuaji na maendeleo ya mtoto.
Kwamba maziwa ya mama husagwa na kumeng’enywa kwa urahisi na kutumika kwa ufanisi zaidi kuliko maziwa ya kopo au maziwa ya kawaida ya wanyama. Hivyo hata kama yanatoka kidogo sana wakati mwingine hicho ndicho kiwango sahihi cha maziwa anayopaswa kupata mtoto.
Tena mama asimwage maziwa yake ya mwanzo yenye rangi ya njano (Colostrum). Maziwa haya humpatia mtoto kingamwili dhidi ya magonjwa mbalimbali, ambazo mtoto huwa hajazaliwa nazo.
Mama aanze kunyonyesha ndani ya saa moja baada ya kujifungu kwani hii itasaidia kuzalisha homoni zinazotengeneza maziwa mwilini mwako. Vilevile mama aanze kula vyakula vitavyosaidia kuzalisha maziwa kwa wengi kama uji, supu mtori. Anaweza kuongeza viungo vyenye virutubishi kwenye vyakula hivi kama pilipili manga, mdalasini, hiliki, tangawizi na mbegu za maboga.
Anyonye mara ngapi kwa siku? Mtoto anyonyeshwe kila anapohitaji kunyonya na kuonyesha dalili za kuwa na njaa kama vile kuvuta midomo, kunyonya midomo, na kadhalika.
Kadiri mtoto anavyonyonya mara kwa mara anasaidia kuchochea uzalishaji wa maziwa zaidi toka kwa mama yake. Tena ili maziwa yazalishwe kwa wingi hakikisha mama hana mawazo.
Msongo wa mawazo na hata kutojiamini kuwa maziwa yake yanatosha na hata magonjwa hupunguza uzalishaji wa maziwa. Iwapo mama hashindi kutwa na mtoto anaweza kukamua maziwa yake na kumpatia mtoto.
Kukamua maziwa kutamsaidia pia mtoto mgonjwa anaeyeshindwa kunyonya ziwa lake kuendelea kupata maziwa. Kabla ya kuanza kukamua maziwa hakikisha mikono imeioshwa na maji safi na salama yanayoririka na kwamba ziwa ni safi na kavu.
Usafi wa vyombo utakavyoweka maziwa yaliyokamuliwa ni muhimu sana kuzingatiwa.
Unapokamua maziwa hakikisha mama umekaa au kusimama eneo huru na mwili wako umepumzika vizuri ili kuruhusu maziwa kutoka vizuri na kwa wingi. Unapoanza kukamua maziwa yanaweza yasitoke. Usikate tamaa. Endelea kukamua taratibu.
Tafiti nyingi zimeonesha kuwa kunyonyesha ni jambo muhimu na hasa kwa kipindi cha miezi sita ya maisha ya mtoto. Maziwa ya mama yanamsaidia mtoto kujiepusha na magonjwa mengi tu ambayo yanayosababisha vifo vingi vya watoto wachanga.
Kunyonyesha kunakuza ubongo na akili za mtoto huku kwa upande wa mama kunyonyesha hupunguza hatari ya magonjwa ya saratani ya kizazi na saratani za matiti.
Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org.