LONDON,UINGEREZA

KATIBU  Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema janga la COVID-19 limevuruga utalii duniani kote na kuleta masaibu mengi.

Guterres akizungumza kwa njia ya video alisema utalii ni miongoni mwa sekta muhimu zaidi ulimwenguni na sekta hiyo inatoa ajira kwa mtu mmoja katika kila watu kumi duniani huku ikitoa riziki kwa mamilioni zaidi ya watu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alisema sekta ya utalii inakuza uchumi na kuwezesha nchi kustawi mbali na kuwezesha watu kuendeleza utajiri wa kiutamaduni wa asili na kuwaunganisha.

Alisema utalii wenyewe ni moja ya maajabu ya ulimwengu na hivyo inaumiza kuona jinsi ambavyo utalii uliharibiwa na janga la COVID-19.

Akieleza tathimini ya athari ya COVID-19 kwa utalii, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alieleza kuwa katika miezi mitano ya mwanzo wa mwaka huu wa 2020, zaidi ya nusu ya watalii wanaowasili kimataifa walipungua na hivyo dola bilioni 320 katika mauzo ya nje kutokana na utalii zilipotea.

Aidha Guterres alieleza kuwa kwa jumla, ajira za moja kwa moja milioni 120 katika za utalii ziko hatarini.

Wengi wako kwenye sekta za uchumi usio rasmi au katika biashara ndogondogo, ndogo na za kati, ambazo huajiri idadi kubwa ya wanawake na vijana. Alisisitiza kuwa, janga hili ni mshtuko mkubwa kwa uchumi ulioendelea, lakini kwa nchi zinazoendelea ni dharura, haswa kwa nchi nyingi ndogo za visiwani zinazostawi na nchi za Afrika