PYONGYANG,KOREA KASKAZINI
JOPO la wataalamu wa Umoja wa Mataifa linasema kuwa Korea Kaskazini inavipuuza vikwazo cha Umoja huo kwa kutanuwa programu ya silaha za nyuklia na makombora ya masafa marefu.
Likiwasilisha ripoti yake kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, jopo hilo lilisema kwamba Korea Kaskazini inaendelea kusafirisha makaa ya mawe na kuingiza bidhaa za mafuta ya petroli kinyume na sheria.
Kwa mujibu wa wataalamu hao waliopewa jukumu la kufuatilia vikwazo dhidi ya nchi hiyo, Korea Kaskazini ilizidisha mara mbili vitendo vyake vya kupuuza vikwazo hivyo kwenye robo ya kwanza ya mwaka huu.
Sehemu ya ripoti hiyo iliyoonekana na shirika la habari la Associated Press inasema kuwa Korea Kaskazini ilifanikiwa pia kukwepa vikwazo kupitia mashambulizi ya mtandaoni yaliyowalenga maofisa wa nchi wanachama wa Baraza la Usalama na wajumbe wa jopo lenyewe.