DAMESKI,SYRIA

MKUU  wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na Ugaidi Vladimir Voronkov amesema zaidi ya wapiganaji 10,000 wa kundi la itakadi kali linalojiita Dola la Kiislamu, IS, bado wanaendeleza operesheni zao nchini Iraq na Syria.

Voronkov aliliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa wapiganaji wa IS wanafanya shughuli zao kwa uhuru ndani ya nchi hizo mbili, miaka miwili tangu kundi hilo lilipoteza udhibiti kamili wa maeneo iliyokuwa ikiyashikilia.

Kwa mujibu wa ofisa huyo wa Umoja wa Mataifa, makundi ya itikadi ya  kali yalikusanyika upya na sasa yanaendesha operesheni hadi nje ya mipaka ya mataifa yaliyo kwenye machafuko ya Iraq na Syria.

Voronkov alionya kuwa propaganda za kundi la IS zinaendelea kupata wafuasi kwenye maeneo mengi duniani huku ikiwemo barani Afrika hususani kwenye mataifa ya Mali, Nigeri na Burkina Faso.