MOSCOW,URUSI

WIZARA ya mambo ya kigeni ya Urusi imesema inaona nafasi ndogo sana ya kufikia makubaliano na Marekani kuhusu mustakabali wa mkataba wa kudhibiti hazina ya silaha za nyuklia kwa pande hizo mbili.

Naibu Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Ryabkov aliliambia shirika la habari la Interfax kwamba nafasi ya kufikia makubaliano inapungua kila siku.

Aliongeza kuwa hawaoni Marekani ikiachana na msimamo wake kwamba ni lazima China ihusike katika majadiliano ya siku za usoni huku akisema bado Marekani inaiwekea Urusi Masharti magumu.

Matamshi ya Ryabkov yalikuja kufuatia duru ya hivi karibuni ya mazungumzo mjini Vienna ya mkataba mpya wa makubaliano hayo yanayofahamika kama START yaliotazamwa kama mazungumzo ya mwisho makubwa baina ya mataifa hayo mawili kuhusu mikataba ya udhibiti wa silaha.

Muda wa mwisho mpango wa sasa wa kudhibiti silaha hizo za nyuklia unatarajiwa kufikia mwisho ndani ya miezi sita.