NA KHAMISUU ABDALLAH

KIJANA wa miaka 45 mkaazi wa Fuoni Migombani wilaya ya Magharibi ‘B’ Unguja, amefikishwa mahakamani kwa kujifanya Ofisa usalama wa Taifa na kuwatapeli watu mamilioni ya shilingi kwa madhumuni ya kuwatafutia ajira katika taasisi hiyo.

Mshitakiwa huyo alitambulika kwa jina la John Samuel Manga, ambae alifikishwa katika mahakama ya wilaya Mwanakwerekwe kujibu tuhuma hizo.

Akiwa mbele ya Hakimu Mdhamini Mohammed Subeit, Mwendesha Mashitaka, Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Mohammed Haji Kombo, alimshitaki mshitakiwa huyo kwa makosa mbali mbali ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Kosa la kwanza aliloshitakiwa nalo ni la kujifanya ofisa wa umma, ambalo ni kinyume na kifungu cha 308 (b) cha sheria namba 6 ya mwaka 2018 sheria za Zanzibar.

Wakili huyo wa serikali alidai kuwa, Mei 17 mwaka huu majira ya saa 4:00 za asubuhi huko skuli ya Mnemonic Academy, kwa udanganyifu alidaiwa kujifanya mtumishi wa umma katika tasisi ya usalama wa taifa na kujifaya ana uwezo wa kumpatia ajira Abubakar Ali Mohammed, katika tasisi hiyo.

Makosa mengine ni kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, kinyume na kifungu cha 299 cha sheria namba 6 ya mwaka 2018 sheria za Zanzibar.

Ilidaiwa kuwa siku hiyo hiyo saa 5:00 majira ya asubuhi katika skuli hiyo, alijipatia shilingi 280,000 kutoka kwa Abubakar, kwa lengo la kumpatia kazi katika tasisi ya Jeshi la Uhamiaji, huku Mei 18 saa 4:00 asubuhi hapo hapo skuli, alijipatia shilingi 180,000 kutoka kwa mlalamikaji huo kwa lengo la kumfanyia pasi ya kusafiria katika mfumo wa kielektronik, ambapo hakumfanyia pasi hiyo wala kumrejeshea fedha zake.

Mbali na kosa hilo, pia ilidaiwa kuwa Mei 22 mwaka huo huo majira ya saa 4:00 asubuhi katika skuli hiyo, pia alijipatia shilingi 500,000 kutoka kwa mlalamikaji huyo kwa lengo la kumnunulia vifaa vya mazoezi.

Sambamba na kosa hilo, Julai 3 majira hayo hayo alijipatia ‘laptop’ moja aina ya Lenovo yenye thamani ya shilingi 350,000 pamoja na kamera moja aina ya Conon yenye thamani ya shilingi 120,000 kutoka kwa mlalamikaji huyo, kwa lengo la kutumia katika mazoezi ya ajira ya Uhamiaji ambapo vitu vyote hivyo havikutumika wala kumrejeshea wenyewe, kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Mbali na mlalamikaji huyo, mshitakiwa John Julai mwaka huu siku na saa tofauti, alijipatia shilingi 2,590,000 kutoka kwa Asha Omar Hamed, kwa lengo la kumpatia kazi katika tasisi ya usalama wa taifa na hakumpatia kazi hiyo wala kumrejeshea fedha zake, kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Mshitakiwa huyo aliposomewa makosa yake aliyakataa na kuiomba mahakama impatie dhamana, huku upande wa mashitaka ukidai kuwa upelelezi wake tayari umeshakamilika na kuomba kupangiwa tarehe nyengine kwa ajili ya kuwasilisha mashahidi.

Wakili Mohammed akizungumzia suala la kupatiwa dhamana mshitakiwa huyo, alisema hana pingamizi ikiwa mshitakiwa huyo atakuwa na wadhamini madhubuti watakaohakikisha kila tarehe ya kesi mshitakiwa anafika mahakamani.

Hakimu Mohammed alikubaliana na ombi la upande wa mashitaka na kuiahirisha kesi hiyo hadi Agosti 11 mwaka huu na kuamuru upande wa mashitaka kuwasilisha mashahadi siku hiyo.

Mahakama ilimtaka mshitakiwa huyo kujidhamini mwenyewe kwa maandishi kwa shilingi 5,000,000 na kuwasilisha wadhamini wawili, ambao kila mmoja atamdhamini kwa kima hicho hicho cha fedha za maandishi, pamoja na kuwasilisha kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi na barua za Sheha wa Shehia wanazoishi.

Mshitakiwa huyo alishindwa masharti hayo na amepelekwa rumande hadi tarehe nyengine aliyopangiwa mahakamani hapo.