Na Amina Omari, BAGAMOYO
TANZANIA imebarikiwa kuwa na vivutio vingi vya utalii ikiwemo wanyama ndege na viumbe hai ndio maana iliamua kutenga zaidi ya robo ya ardhi yake kwa ajili ya mbuga na hifadhi za taifa za wanyama.
Lengo ikiwa ni kuendeleza utalii katika maeneo hayo ili kuinua kujiongezea kipato na kuinua pato la taifa kupitia wageni na wananchi wanaotembelea vivutio hivyo.
Kutokana na umuhimu huo katika kipindi cha utawala wa awamu ya tano ya rais John Magufuli kumekuwa na jitihada kubwa za kufanya uwekezaaji kwenye sekta ya utalii kuwa wa tija zaidi.
Jitihada hizo ni pamoja na kuboresha miundombinu, kutangaza vivutio vilivyoko kimataifa, pamoja na kuitumia watu maarufu duniani kwa ajili ya kutangaza vivutio vyetu ili kuvuta watalii wengi.
Hata hivyo, licha ya Tanzania kuwa na hifadhi nyingi lakini Hifadhi ya Taifa ya Saadani ni miongoni mwa hifadhi pekee katika nchi za Afrika ya Mashariki ambapo lina eneo la nyika na bahari.
Hifadhi hiyo ipo katikati ya miji ya kihistoriaya Bagamoyo, Pangani na Zanzibar ambayo ilishamiri kwa biashara ya utumwa,
Hifadhi hiyo inasifika kwa kuwa na idadi kubwa ya wanyama kama Tembo, Twiga, Mbogo, Ngori, Simba, Chui na aina mbalimbali ya swala, tumbili pamoja na ndege.
Afisa Uhifadhi Hifadhi ya Saadani, Prisca Lyimo, alisema kuwa sekta ya utalii katika miaka ya hivi karibuni imepata msukumo mkubwa kutokana na juhudi kubwa zinazofanywa na serikali kupitia wizara husika katika kutangaza vivutio vya utalii.
Alisema hatua hiyo imewezesha kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi za Tanzania kuongezeka mara dufu kutokana na juhudi kubwa zinazochukuliwa na serikali.
Alisema kuwa kuna mwitiko mkubwa wa watalii kutembelea hifadhi zilizopo kanda ya Mashariki kutokana na uboreshwaji wa miundombinu ya barabara umesaidia kwa kiasi kikubwa kwani sasa maeneo hayo yanaweza kufikika kwa urahisi bila ya shida.
Kwa upande wake Afisa utalii wa hifadhi hiyo, Athuman Mbae, alisema kwa kipindi cha miaka minne mwitikio wa watalii kutembelea hifadhi ya Saadani umekuwa ni wa kiwango kikubwa.
Akitoa takwimu za idadi ya watalii, Mbae alisema kuanzia mwaka 2015 jumla ya watalii 15,000 walitembelea hifadhi hiyo lakini mpaka mwishoni mwa mwaka 2019 jumla ya watalii 22,920 walitembelea hifadhi hiyo.
Alisema kuwa maboresho ambayo yanaendelea kufanywa na serikali ndio yamesaidia kukuza sekta ya utalii hapa nchini kwani sasa watalii wanaweza kufika kwa haraka katika hifadhi hizo nchini.
Alisema kuwa ukiwa katika hifadhi hiyo mtalii anaweza kufanya utalii wa mbugani kwa kutumia magari wakati wa mchana, sambamba na utalii wa usiku ambao huu ni maalum kwa ajili ya kujionea wanyama ambao hawaonekani nyakati za jua kali.
Aidha alisema kuwa utalii mwingine wa mapumziko katika fukwe safi za bahari ya Hindi ikiwemo kushuhudia mazalio ya kasa wa kijani wanapoanguwa, Sambamba na michezo mbalimbali ya baharini.
Mbae aliyataja baadhi ya mafanikio sekta ya utalii ni uanzishwaji wa reli Dar kwenda Moshi ambao husaidia kuongeza idadi ya watalii wanaopanda reli hiyo kujionea maajabu mbalimbali ya hifadhi hiyo.
Kuhusiana na mradi wa ujirani mwema, Mbae alisema kuwa ili wananchi wamenufaike na hifadhi hiyo ya Taifa ya Saadani kwa kuwa wamepatiwa miradi mbalimbali ya kimaendeleo iliyotumia kiasi cha zaidi ya shilingi Bilioni 1.1 kwa vijiji 11 Kati ya 18 vinavyozunguka hifadhi hiyo.
Alisema Hifadhi imetekeleza jumla ya miradi 25 iliyoko kwenye sekta za Afya, Elimu, Maji na Mazingira imefadhiliwa na hifadhi hiyo kwa kushirikiana na wananchi.
Kwa upande wake Mtendaji wa Kijiji cha Saadani, Martina Ngulei, alisema kuwa hifadhi hiyo imeweza kusaidiana na wananchi katika kutatua kero mbalimbali ambazo zilizoikabili vijiji hivyo.
Aliongeza kuwa licha ya misaada ya kimaendeleo lakini wameweza kupatiwa elimu ya namna ya kuishi na wanyama kwani kulingana na mazingira ya hifadhi hiyo wanyama nao wamekuwa ni sehemu ya jamii.
Nao baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Saadani walisema kuwa kuishi kwa jirani na hifadhi kumekuwa ni neema kubwa kwao kwa kipato sambamba na fursa za biashara.
Mbuga ya Saadani ni miongoni mwa mbuga muhimu zilizopo Tanzania kiasi kwamba ina umuhimu wa pekee hasa kutokana na kupatikana bahari tofauti na mbuga nyengine zenye maziwa na mito.