NA TATU MAKAME

HIFADHI ya Taifa Jozani na Ghuba ya Chwaka iliyopo Mkoa wa Kusini Unguja imeanza kupokea wageni wanaotembelea eneo hilo baada ya kusita kwa shughuli za kitalii kwa zaidi ya miezi mitatu kutokana na ugonjwa wa corona.

Akizungumza na Zanzibar Leo, msaidizi mkuu wa hifadhi hiyo ambae pia ni ofisa uhifadhi na ikolojia, Mzee Khamis Mohamed alisema wageni kutoka nchi mbalimbali duniani wameanza kutembelea eneo hilo na kuona vivutio vilivyomo.

Alisema wageni ambao walisita kwa kipindi hicho wameanza kurudi mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu, ingawaje wageni wanaotembelea eneo hilo kwa sasa idadi yao ni kidogo.

“Ingawa wageni hawajachanganya, lakini tunapokea wageni kutoka nchi mbalimbali duniani wanaokuja kuangalia vivutio vilivyo kwenye hifadhi yetu”, alisema.

Aidha alisema wamepata faraja kuanza kupokea wageni kwani hifadhi hiyo inategemea watalii. “Kurudi kwa harakati za utalii tumepata faraja kwani huduma nyingi zinategemea kuwepo kwa utalii hata uchumi wetu unategemea”, alieleza.

Akizungumzia mikakati ambayo wanaiendeleza alisema kuzingatia masharti na kanuni za afya kwa kuhakikisha kila mgeni anaeingia ananawa kwa kutumia vitakasa mikono na kuvaa barakoa kila anapotembelea maeneo ya hifadhi.

Kuhusu utalii wa ndani alisema bado idadi ya wageni wanaoingia ni ndogo, hivyo aliwataka wananchi kutembelea maeneo hayo kwani watajifunza mambo mbalimbali.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Jumuiya ya uhifadhi ya Taifa Jozani Awesu Shaaban Ramadhani, alisema wamefarajika kurejea tena kwa harakati za utalii na kwamba shughuli zao wanazozifanya zitaendelea vizuri ingawa wao wanahusika na shughuli za jamii ikiwemo kuhamasisha kulinda misitu.

Aliwataka wageni wanaotembelea maeneo hayo kufuata masharti ili kujikinga na ugonjwa huo.