NA ARAFA MOHAMED
ALIESHINDWA kuvaa beji ya utingo, amefikishwa katika mahakama ya mwanzo Mwanakwerekwe kujibu tuhuma hizo.
Mshitakiwa huyo ni Ramadhan Hassan Juma (22) mkaazi wa Bububu Unguja, alifikishwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Nassim Fakih Mfaume na kusomewa shitaka lake na Mwendesha Mashitaka, Koplo wa Polisi Salum Ali.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, mshitakiwa huyo akiwa utingo wa gari yenye namba za usajili Z 980, inayokwenda njia namba 537, akitokea upande wa Amani kuelekea Mwanakwerekwe katika mzunguko wa barabara (round about), alipatikana akiwa hakuvaa beji ya utingo, jambo ambalo ni kosa kisheria.
Kushindwa kuvaa beji ya utingo ilidaiwa kuwa ni kinyume na kifungu cha 99 (6) (14) ya namba 46 ya mwaka 2005, vya kanuni ndogo za vyombo vya moto vinavyohusiana na biashara zilizofanywa kinyume na kifungu cha 80 cha sheria namba 7 ya mwaka 2003 sheria za Zanzibar.
Tukio hilo alidaiwa kulitenda Agosti 2 mwaka huu, majira ya saa 12:20 asubuhi huko Mwanakwerekwe sehemu ya kukoshea magari (car wash) Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Aliposomewa shitaka lake hilo mshitakiwa huyo, alilikubali na kuiomba mahakama imsamehe, ombi ambalo halilikubaliwa mahakamani hapo.
Mahakama ilimtia hatiani mshitakiwa huyo, na kumuona ni mkosa kisheria na kumpa adhabu ya kulipa faini ya shilingi 25,000, na akishindwa atatumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa miezi miwili, ili iwe fundisho kwake na kwa wengine watakao dharau sheria za usalama barabarani.
Mshitakiwa Ramadhani alilipa faini hiyo ili kujinusuru kwenda Chuo cha Mafunzo kwa muda huo kama alivyo amriwa na Hakimu Nassim.