ANKARA,UTURUKI

UTURUKI imesema iko tayari kufanya mazungumzo na Ugiriki kuhusiana na mvutano unaongezeka juu ya hifadhi ya gesi na mafuta katika eneo la bahari ya Mediterranea ulioshuhudia mataifa hayo mawili yakitunishiana misuli kwa kufanya luteka za kijeshi.

Waziri wa Mambo ya kigeni wa Uturuki Mevlut Cavusoglu alisema nchi yake inakubali pendekezo la kuwepo mazunguzo yasiyo na masharti juu ya uwezekano wa kugawana kwa usawa rasilimali zilizopo kwenye eneo hilo la bahari.

Msimamo wa Uturuki ulitolewa baada ya juhudi za waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Heiko Maas ambaye aliezitembelea Uturuki na Ugiriki kujaribu kutuliza mzozo unaofukuta.

Kwa upande wake Ugiriki nayo ilisema itakubali kushiriki majadiliano ya kutafuta suluhu ya mzozo unaondelea lakini siyo chini ya vitisho kutoka Uturuki.