NA MADINA ISSA

UMOJA wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), umelaani matamko yanayotolewa na baadhi ya viongozi wa siasa ambayo yana viashiaria vya uvunjifu wa amani wakati huu wa kuelekea kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu.

Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar, Mussa Haji Mussa, aliyasema hayo, alipokuwa akitoa tamko la Umoja wa Vijana wa CCM huko ofisi kwake Gymkana kufuatia viongozi hao kutoa matamko baada ya wagombea wa nafasi ya ubunge kuwekewa pingamizi.

Alisema, kuna viongozi wanatoa kauli zilizokuwa hazikubaliki katika kipindi hichi cha kuelekea uchaguzi, jambo ambalo linapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria.

Alisema kauli hizo zimetosha kwani zimekuwa zinakwenda kinyume na matamko ya vyama vya siasa ambalo limetiwa saini na vyama vyote na kuridhiwa na tume ya uchaguzi NEC.

Aidha alisema, suala la wagombea kuwekewa pingamizi lipo kisheria kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi kifungu NO.  51 (1) cha sheria ya uchaguzi namba 4 ya mwaka 2008, ambapo mgombea yoyote wa chama anaweza kuwekewa pingamizi.

“Hata mgombea wa urais kwa tiketi ya Chama chetu CCM, Dk John Pombe Magufuli, pamoja na mgombea urais kwa tiketi ya CUF, Prof. Lipumba waliwekewa pingamizi na kusikilizwa na baada ya kubainika halina mantiki lilitupiliwa mbali” alisema.

Hivyo, aliwaomba viongozi wa dini kulaani matamshi yanayotolewa na viongozi hao wa kisiasa ambayo yamekuwa yakiashiria uvunjifu wa amani ya taifa.

Sambamba na hayo, aliwataka wanaCCM na wazanzibari kuhakikisha wanaendelea kulinda amani iliyopo kwa gharama yoyote ile ili taifa liweze kubaki salama.