NA ASIA MWALIM
WATUHUMIWA 25 wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu ikiwemo wizi, unyang’anyi na uporaji wa kutumia silaha za jadi wametiwa mbaroni na jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi.
Kamanda wa Polisi Mkoa huo Awadh Juma Haji, aliyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari huko ofisini kwake Mwembe Madema Mjini Zanzibar.
Kamanda huyo alisema katika sherehe za Eid el hajji, Jeshi la Polisi Mkoa huo lilijipanga katika kukabiliana na vitendo vya kihalifu na kwamba operesheni zalizofanywa katika maeneo mbalimbali zimezaa matunda kwa kuwakamata wahalifu hao.
Kamanda Awadh alisema watuhumiwa hao walikamatwa Agosti 3 mwaka huu wakiwa na vitu vya aina mbalimbali vya wizi simu 44 za mkononi zikiwemo ‘smartphone’ 28 zenye rangi tofauti, simu ndogo 16, mikoba ya kike minne na miwani pea moja.
Alifahamisha kuwa wananchi wawe tayari kufika kituoni na kutoa ushahidi ili watuhumiwa waweze kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa mahakamani.
Vilevile jeshi hilo limetoa wito kwa wananchi wote ambao wamewahi kuibiwa simu na mikoba wafike ofisi ya Mkuu wa upelelezi Mkoa wa Mjini Magharibi iliyopo kituo cha Polisi Madema ili kuweza kuitambua.
Aidha kamanda huyo alisema idadi kubwa ya wahalifu hao waliokamatwa katika matukio hayo inaonyesha kuwa sio wakaazi wa Zanzibar na kwamba wanatoka nje ya nchi.
Sambamba na hayo, alisema Jeshi la Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja litakua na msako endelevu ili kuhakikisha linadhibiti wahalifu wanaojihusisha na matukio yote ya kihalifu, hivyo aliwataka watu wenye tabia hiyo kuacha haraka kwani uhalifu hauna nafasi katika mkoa huo.
Alisema kuwa watuhumiwa hao watafikishwa Mahakamani kwa ajili ya hukumu baada ya upelelezi kukamilika watafikishwa sehemu husika.