NA KHAMISUU ABDALLAH

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar kupitia ofisi ya kadhi mkuu wa Zanzibar imeshauriwa kulitilia mkazo suala la wanandoa kujifunza katika vyuo vya maadili ya ndoa vilivyoanzishwa nchini ili kupunguza wimbi la talaka.

Ushauri huo umetolewa na Mwalimu Mkuu wa Chuo cha Ndoa kutoka Jumuiya ya Maimam Zanzibar, Ali Abdalla Amour, wakati akizungumza na Zanzibar Leo ofisini kwake Majestik.

Alisema ikiwa ofisi ya kadhi italitilia mkazo suala hilo kama lilivyo suala la vyeti vya kupima HIV basi kwa kiasi kikubwa litaweza kupunguza migogoro ya ndoa hapa Zanzibar.

Alisema bado jamii haijawa na muamko wa watoto wao kujiunga na vyuo hivyo hali ambayo inapelekea kuongezeka kwa migogoro ya ndoa katika jamii.

“Serikali ifikirie kuona mtu harusiwi kuingia katika ndoa mpaka awe amepata mafunzo ya ndoa ili kusaidia watu kudumu katika ndoa zao,” alisema.