NA MWANAJUMA MMANGA

KATIBU Mkuu wa Baraza la Mapinduzi na Kiongozi, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee anatarajia kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya vijana kitaifa yanayotarajiwa kufanyika leo kiwanja cha kufurahishia watoto Kariakoo mjini Zanzibar.

Ofisa miradi vijana, Sheila Makungu Mwinyi kutoka Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo, aliyasema hayo wakati akizungumza na mwandishi wa gazeti hili huko ofisini kwake Migombani wilaya ya Mjini.

Alisema siku hiyo kitaifa huadhimishwa kila ifikapo Agosti 12 ya kila mwaka na chimbuko lake limetokana na wazo la vijana lililopendekezwa katika mkutano uliofanyika mjini Vienna nchini Austria, mnamo mwaka 1991.

Aidha alisema siku hiyo ulifanyika mkutano wa mwanzo duniani na kuhudhuriwa na mawaziri wenye dhamana kwa vijana.

Alisema azimio la kupitishwa siku hiyo kila ifikapo Agosti 12 ya kila mwaka ni siku ya vijana kitaifa liliridhiwa rasmi na baraza kuu la 54 la Umoja wa mataifa Desemba 17 mwaka 1999.

Ofisa huyo alisema katika maadhimisho hayo kutahudhuriwa na viongozi wa wizara mbali mbali, taasisi za vijana na mabaraza ya vijana.

Pia kutakuwa na burdani mbali mbali za vijana, ikiwemo ngoma za asili, muziki wa kizazi kipya, uwasilishaji wa mada zinazohusu vijana pamoja na uchangiaji damu kwa hiyari, hivyo aliwataka wananchi na vijana kushajiika na kushiriki kwa wingi ili kufikia malengo hayo.