NA TATU MAKAME

MKUU wa Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja, Hassan Ali Kombo, amesema vijana wanauwezo mkubwa wa kutoa mawazo na maamuzi endapo watashirikishwa ipasavyo katika shughuli za kimaendeleo.

Akihutubia huko katika ukumbi wa Mkutano Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini Unguja Mkokotoni Mkoa wa Kaskazini Unguja, katika kongamano lililowashirikisha vijana kutotumiwa vibaya nafasi zao katika kipindi hiki kinachoelekea Uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

Akizungumza kwa niaba yake Msaidizi Mipango na fedha wa halmashauri hiyo Haji Jabir Haji, alisema vijana ni nguvu kazi ya Taifa na wanafursa nyingi za kufanya mambo ya maendeleo zikiwemo za kiuchumi na kijamii hivyo si vyema kundi hilo likajihusisha na vitendo vya uvunjifu wa amani katika kipindi hiki.

Alifahamisha kuwa endapo vijana watajihusisha na vitendo vya uvunjifu wa amani watalifanya Taifa kuingia katika hali mbaya kiuchumi, na kuingia katika machafuko hivyo ni jukumu lao kutumia nafasi hiyo vizuri katika kipindi hiki.

 Ofisa mipango wa wilaya hiyo ya Abdulmajid Ramadhan akitoa mada juu ya ushiriki na ushirikishaji wa vijana wakati wa kampeni ,wakati wa uchaguzi mkuu na wakati wa  matokeo ya uchaguzi, aliwasisitiza vijana kutojihusisha na vitendo vya vurugu au uchochezi wakati wa kwenda au kurudi katika mikutano ya kampeni .

Aidha liwaasa vijana kutochukua silaha wakati wa kushiriki mikutano ya kampeni katika kipindi hicho kwani wanaweza kujiingiza katika matatizo.

Nae Ibrahim Hassan Kombo kutoka Ofisi hiyo aliwaonya vijana wenzake kuchagua viongozi wenye kuendelea kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kutokubali kutumiwa na viongozi wasioitakia mema nchi yao.

Nao Wasila Kombo Tano na Mbarouk Suleiman, wakizungumza kwa niaba ya vijana wenzao walisema watakuwa mabalozi wazuri kwa wenzao kuwaelimisha juu ya madhara ya uvunjifu wa amani katika jamii hasa kipindi hiki.

Hata hivyo walisema wafikishe elimu hiyo kupitia mabaraza ya vijana, jumuiya na vikundi mbali mbali vilivyomo  ndani ya Shehia zao kupitia mafunzo waliyoyapata katika kongamano hilo.

Kongamano hilo lenye kauli mbiu ”Kuwajumuisha vijana katika kuchukua hatua Ulimwenguni”hufanyika kila ifikapo tarehe 12 Agost ya kila mwaka ambapo katika wilaya hiyo maadhimisho hayo yalifanyika Mkokotoni na liliwashirikisha zaidi ya vijana 200 wa wilaya hiyo.