NA MWANTANGA AME

VIJANA ni moja ya nguzo muhimu ya maendeleo katika nchi yoyote duniani ambayo serikali iliopo madarakani hutegenea nguvu za kundi hilo katika suala zima la uzalishaji.

Kundi la vijana mara nyingi limekuwa na matumaini makubwa ya maisha mazuri katika uhai wao wote, jambo ambalo huwafanya kujiingiza katika shughuli mbali mbali za kijamii.

Moja ya shughuli ambazo wamekuwa wakijiingiza ni za kisiasa, ambapo hujiunga na vyama tofauti kwa dhamira mbali mbali zikiwemo ya kujiletea maendeleo yao.

Kutokana na dhamira hiyo ya vijana imewafanya viongozi wengi waliokaa madarakani kuona umuhimu wa kuyajali makundi hayo, kwa kuwaekea fungu la kuwahudumia katika bajeti zao za kila mwaka.

Hii ni kutokana na wengi wao kukumbwa na tatizo la ajira kunakosababisha na mambo mbali mbali, kiasi ambacho wale wasioapata fursa za kuajiriwa serikalini huamua kujiingiza katika mambo mbali mbali yakiwamo maovu.

Ingawa huo ndio mtazamo wa vijana, lakini serikali imekuwa ikijitahidi kuwafanyia mabadiliko yanayoweza kuwapa matumaini ya maisha mapya, jambo ambalo wamewekewa za sera ya kuwaendeleza kimaisha, kimasomo na maakuzi mema.

Sera hii, husimamiwa na serikali moja kwa moja ambapo hivi sasa kwa Zanzibar, ipo chini ya utawala wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein.

Dk. Shein, katika utawala wake ameweza kuyapatia huduma mbali mbali makundi ya vijana kiasi ambacho anaondoka madarakani wamemkubali kama amewajali katika kuyapatia huduma bora.

Makundi haya ya vijana hivi sasa yamepata matumaini mapya ya kuja kwa Mgombea mpya wa Chama cha Mapinduzi CCM ambaye anatarajiwa kuwa ni Dk. Hussein Hassan Mwinyi.

Vijana wanajenga matumaini kwa Mgombea huyu kutokana na sababu mbali mbali za utumishi wake alianza nao katika serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa kuweza kufanyakazi na Marais watatu tofauti ndani ya kipindi cha miaka 15 aliyokaa madarakani.

Matumaini hayo yanakuja kutokana na mtazamo wake aliouonesha kwa kutangaza hadharani kama yuko tayari kuyatumikia makundi yote ya kijamii yakiwemo ya vijana.


Pamoja na hilo, Dk. Hussein Mwinyi katika ahadi zake alizozitoa katika mikutano yake ya Unguja na Pemba, alisema kwama yuko tayari kuyaenzi Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 kwani suala hilo atalifanya kwa uhakika.

Jambo jengine ambalo aliliahidi katika mikutano yake hiyo ni kudumisha Muungano kwa kuufanya kuwa ni wa aina yake, kwani unatiliwa mfano duniani kote kiasi ambacho viongozi wake wamekuwa na Imani ya kuwafanyia mambo mengi watanzania.

Kuna suala kubwa, alisema atalolisimamia ni la amani kwani ni moja ya jambo linaloifanya Tanzania kupata maendeleo kwani nchi nyingi za jirani hakuna Amani na amemshukuru sana Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein kwa kuongoza nchi kwa amani.

Alisema kwamba hilo ni jukumu lake la kuhakikisha amani inadumu na ni lazima wadumishe umoja, ili kusiwe na Upemba na Unguja, kusiwe na Ukusini na Ukaskazini kwani wote ni Wazanzibari.

Suala la ajira, Dk. Mwinyi ameahidi kulishughulikia hasa kwa vijana na amempongeza Rais Dk. Shein na viongozi wote wa serikali na chama na atahakikishe alipoachia yeye atapaendeleza.

“Nitaendeleza miundombinu, huduma za jamii, ustawi wa watu, maendeleo ya jamii, afya, elimu, na yote yanayogusa watu, Nitahakikisha Mzazibari anakua na maisha bora” alisema.


“Ukitaka kuyafanya hayo, lazima uwajibike Huwezi kuwa na program kukawa na wala rushwa, wabadhirifu, Wazembe Sitokuwa na huruma kwa wenye tabia hizo, Serikali itafanya kazi kwa maslahi ya Wazanzibari wote”.


“Wapo wanaosema Mwinyi ni mpole. Mimi Nasema wataniewa, nasema haya kwa sababu pengine hamjanisikia nikiongea sana kwenye vyombo vya habari. Sababu kubwa ni kwamba Wizara ya Ulinzi huko mambo yetu ni ya siri hatufanyi hadharani.

Siwezi kusema ila kwa wale wabadhirifu, wala rushwa, wazembe, wasiowajibika, hao watawajibika” alisema.


“Nitasimamia maslahi ya Zanzibar kwenye Muungano, Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya za Kimataifa. Nikwambieni nimeamua nigombee na ili nitakaposhinda dhamira yangu ni moja kuwatumikia Wazanzibari wote”, alisema.


Alisema kwamba wanaposhika dola, atakuja na miradi ya kusaidia Wazanzibari, ikiwemo ajira kwa wote bila ubaguzi hasa kundi la vijana.

Nasema tena kwamba ‘Yajayo yanafurahisha.’ Ni ahadi naichukua mbele ya Mungu na mbele yenu. Nitahakikisha nawahudumia wananchi.


“Sasa na wakati huu nina hakika tunafanya mambo mazuri kwa maisha yetu yawe mazuri Kazi iliyobakia ni kwenda kushika dola na si vyenginevyo. Kwa sasa lililobakia ni umoja mshikamano na ushirikiano ndani ya CCM”, alisema.

Tamko hili la Dk. Hussein Mwinyi, limewapa matumaini vijana wengi katika visiwa vya Unguja na Pemba, ambapo tayari wameanza kutoa maoni yao mbali mbali juu ya suala hilo.

Wananchi Z’bar hasa vijana wajenga matumaini makubwa Dk. Hussein Mwinyi, kwani wameipongeza Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kumchagua Dk. kuwa mgombea wa Urais wa Zanzibar katika uchaguzi Mkuu ujao, kupitia chama hicho.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi hao walisema Halmashauri Kuu inastahili pongezi kwa kuchagua kijana na ataejua matatizo ya wananchi na kuyatatua na kuyaendeleza mazuri yatakayoachwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohammed Shein.

Vijana hao walifahamisha kuwa imani ya wanachama wa Chama cha Mapinduzi na Wazanzibari ipo kwa mgombea huyo Dk. Hussein Mwinyi kutokana na mengi aliyoyafanya katika jimbo alilokuwa akiliongoza na chama chake.

“Imani yetu sisi Wazanzibari hivi sasa ipo kwa Dk. Hussein kwa sababu ndio chaguo la Halmashauri Kuu na sisi tunaamini kwamba atakua kiongozi imara, mchapakazi na asiependa majungu, na anatupa matumaini sisi vijana”, alisema Kassim Issa.

Aidha, alisema kwamba uamuzi ya kikao hicho ni ule uliotukuka, kwani wanaamini kwamba kiongozi aliechaguliwa atakuwa kiongozi imara na mwenye kuleta maslahi bora kwa Wazanzibari.

“Naipongeza Halmashauri Kuu ya CCM kwani imetuchagulia kijana madhubuti ambae tunaamini ataweza kusukuma gurudumu na kutuletea maendeleo makubwa zaidi visiwani mwetu,” alisema Dauhat Saleh.

Dauhat alifahamisha kwamba anaamini waliochukua fomu kuwania nafasi hiyo wote walikuwa wazuri katika kushika madaraka, lakini imewalazimu kuchagua mtu mmoja ambae atakua mzuri zaidi.

Rehema Maulid, alisema kwamba kutokana na maendeleo yalioletwa ndani ya miaka kumi ya uongozi wa awamu ya saba, ni vyema Rais huyo mtarajiwa ahakikishe anayaendeleza mazuri ambayo yameachwa na kiongozi anaeondoka. 

Alimshauri mgombea huyo kuyaendeleza yaliyofanywa na mzazi wake wakati alipokuwa Rais wa Zanzibar na Tanzania ambayo hivi sasa yanawafaidisha vijana wengi katika kupata fursa za kibiashara zinazobadili aina ya maisha yao.

Alisema kwamba kutokana na kushika wadhifa wa Uwaziri katika vipindi tofauti katika Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, wanaamini atakuwa mstari wa mbele kuyaleta mazuri yanayofanywa nchini humo.

Hata hivyo, alifahamisha kwamba wanaamini kuwa Rais huyo mtarajiwa ataleta mageuzi makubwa katika kila sekta kutokana na kupikwa mapema kisiasa na kiutendaji.

Ali Hemed, alisema kwamba maamuzi ya Kamati Kuu wameyapokea kwa moyo mmoja, kwani wanaamini kiongozi aliechaguliwa ataweza kutetea haki za wana CCM na Wazanzibari kwa kuwainua vijana kimaisha.

Hilo alisema linawapa matumaini kutokana na kuwa yeye bado ni kijana, jambo ambalo litampa uwezo mkubwa wa kutambua kwa haraka mahitaji ya vijana wa Zanzibar na nini aweze kufanya ili kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazowakabili katika maisha yao.

Alisema, chama cha Mapinduzi hivi sasa kimeanzisha mabaraza ya vijana kwa lengo la kuweza kukutanisha   vijana wote na kuweza kukisaidia ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na chama  hicho.

Alifahamisha kuwa, Vijana ndio nguvu kazi ya Taifa hivyo ni vyema wakawa wazalendo na nchi yao, na kukipenda chama chao ili kumsaidia Dk. Mwinyi atapoingia madarakani ikiwa ni hatua itayoleta maendeleo yao binafsi  na taifa kwa ujumla.

Katibu wa Umoja wa Vijana Tanzania, Ramadhan Abasi Suleiman (Mcheju) alisema  baada ya kupatikana kwa Mgombea wa CCM Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi, kwa sasa  Tanzania  inaelekea  katika  uchaguzi  mkuu,  hivyo  ni  vyema  kwa vijana  kujitokeza  kwa  wingi  kuona wanatimiza ndoto zao kwa vile wamempata kiongozi ataewajali kutokana na ahadi zake alizozitoa.

Alisema jambo la msingi hivi sasa kwa vijana wataopata nafasi mbali mbali za kugombea uongozi katika  majimbo  yao watapochaguliwa wamsaidie ili kuonesha mashikamano na uzalendo kwa chama chao.

Nae   Mwenyekiti  wa Umoja wa Vijana, Wilaya  ya  Amani,  Hassan  Abdallah  Said,  alisema  kuwa  watahakikisha wanawahamasisha  Vijana wa chama hicho, kujitokeza kwa  wingi  katika  kukipigia  kura  chama  hicho,  ili kiweze kushinda katika uchaguzi mkuu ujao kwani Dk. Mwinyi anauzika.

Alisema matumaini ya vijana ni makubwa kwao kwa vile kuna mambo mengi yatayoweza kubadilishwa katika sekta tofauti na hasa vijana waliopo vijijini kwa vile ndio kundi lililosahaulika kiasi ambacho wameamua kuja mjini kutafuta maisha.

Alisema hivi sasa sehemu kubwa ya mji wa Zanzibar umeelemewa kutokana na kuwapo kwa idadi kubwa ya watu na kundi kubwa ni vijana, jambo ambalo limewafanya kuendelea shughuli zisizorasmi kwao.

Kutokana na hali hiyo, alisema kuja kwa Dk. Mwinyi kunawapa matumaini makubwa ya mabadiliko ya maisha ya vijana, kwani atae mrithi amewaachia msingi mzuri wa kuwaendeleza kwa vile tayari kuna mipango mingi iliyopangwa ndani ya Mabaraza yao katika sekta tofauti ikiwemo ya kilimo cha mboga mboga.

Hivyo basi iko haja kwa vijana kuyaona maeneo hayo yanafaida kubwa kwako na jambo muhimu wa kukipigia kura nyingi Chama cha Mapinduzi, kwa vile tayari kimeshawaonesha dira itayotumiwa katika baada ya uchaguzi mkuu ujao, kwani vijana ni taifa la leo.