WAZEE wetu hawakukosea waliposema mjenga nchi ni mwananchi na mbomoa nchi pia ni mwananchi mwenye, hata hivyo kuna tofauti kubwa sana baina watu wa aina mbili hizi.

Kwa tafsiri yetu mjenga nchi ni mwananchi aliyezaliwa na kufunza uzalendo jinsi ya kuitumikia nchi ya watu wake, huku nafsi yake ikifunzwa kuondokana na tamaa na maslahi binafsi.

Mjenga nchi anatofautiana sana na mbomoa nchi, ambaye naye amefunzwa kila kitu kama mjenga nchi, lakini mafunzo aliyopewa yamekuwa chini kuliko tamaa za nafasi yake.

Hivi sasa kadiri siku zinavyosonga mbele ndipo jamii inaposhuhudia kuporomoka kwa kitu kinachoitwa uzalendo na kupotea kwa mapenzi na nchi kiasi cha kujiuliza kwanini yatokee haya.

Ukichunguza kwa makini unamkuta mfanyaji wa vitendo vilivyokosa uzalendo babu na babu zake, bibi na bibi zake wamezaliwa kukua, kufa na kuzikwa hapa hapa na hawana shaka dhidi ya uzawa wao.

Hatuelewi kitu gani hasa kinawasibu vijana wetu hadi kusababisha kukosa uzalendo na badala yake kuwa wahujumu wa mali za jamii, ikiwemo suala zima la wizi, rushwa na kuharibu mali za umma.

Vijana na wasichana wanapelekwa skuli hadi kufika vyuo vikuu na kufundishwa fani mbalimbali, lakini akeshaajiriwa anatumia nafasi yake kwa maslahi binafsi, huku ndiko kukosa uzalendo.

Katika kujihalalishia uovu wao, baadhi yao wameunda semi walizozipa tafsiri potofu dhidi ya badahi ya mamlaka na taasisi hapa nchini, utasikiwa wakiziita ‘chukua chako mapema’, hii ni semi inayohamaisha wizi na ubadhifu.

Serikali imemuajiri kwa kuamini kuwa utaalamu wake alionao utaongeza ufanisi na kusukuma mbele maendeleo ya taasisi, lakini stashahada, shahada na utaalamu huwekwa pembeni na kinachoendelea ni uhujumu kwenda mbele.

Tumefikia pahala vijana wanaoajiriwa huwa hawana subira, wanachotaka ni japo kwa kutumia njia za mkato, ilimradi baada ya miaka michache ajira aliyoipata iwe imeshamlipa.