KHARTOUM,SUDAN

VIKOSI  vya usalama vya Sudan vililazimika kufyatua mabomu ya kutoa machozi kutawanya maelfu ya waandamanaji, waliokusanyika kwa ajili ya kumbukumbu ya makubalino ya kugawana madaraka huku wakitaka mageuzi ya haraka.

Makubaliano hayo yalifikiwa baina ya muungano wa kiraia na maofisa wa kijeshi,baada ya kiongozi wa muda mrefu Omar al-Bashir kuondolewa madarakani mwaka jana.

Serikali ilisema kuwa inasonga mbele na mageuzi lakini watu wengi wanataka mabadiliko ya kina na ya haraka.

Miongoni mwa madai ya sasa ni kuundwa kwa bunge la mpito, kupangwa upya kwa vikosi vya muungano wa kiraia wa uhuru na mabadiliko pamoja na raia kuchukua usukani wa makampuni yanayoendeshwa na jeshi.

Chama cha wataalamu wa Sudan SPA kilisema vikosi vya usalama vilitawanya waandamanaji baada ya kutaka kukutana na Waziri mkuu Abdallah Hamdok.