NA KIJA ELIAS, MOSHI

WANACHAMA wa Chama Cha Watu wenye Ulemavu wa Viungo (CHAWATA) mkoa wa Kilimanjaro, wamewasimamisha viongozi wao kwa tuhuma za  ubadhilifu na matumizi mabaya ya fedha na madaraka akiwamo Mwenyekiti wa mkoa na Katibu wa chama hicho wilaya ya Rombo mkoani hapa.

Maamuzi hayo yalifanyika kupitia Mkutano Mkuu wa Chawata mkoa uliofanyika mjini Moshi jana, baada ya taarifa ya Katibu Mtendaji Paulo Ndehaki, aliyoisoma mbele ya wajumbe wa kikao hicho, yanayotia shaka.

Ndehaki alisema Mwenyekiti aliyemtaja kwa jina la Kawawa Mwachitiku amekuwa kinara wa tuhuma hizo kwani amekuwa akitumia jina la Chawata kwenda kwa wadau kuomba misaada kinyume na mwongozo wa chama hicho.

“Amekuwa akifanya hivyo kinyume na mwongozo wetu (Chawata), amekuwa akipita kwa wadau kuomba msaada wa hali na mali pia fedha wakati ofisi imekuwa ikimgharimia kila kitu pindi anapokwenda kwenye majukumu yanayohusu chama,” alisema Ndehaki.

Wengine waliosimamishwa ili kupisha uchunguzi wa tuhuma hizo ni Makamu  Mwenyekiti wa Chawata wilaya ya Rombo Bazil Lemunge na Katibu Chawata wilaya ya Rombo Getruda Kimario.

Aidha Ndehaki, alisema mwenyekiti huyo, amekuwa ni kikwazo, hali ambayo imekuwa ikichangia kukidhoofisha chama, kutumia madaraka yake vibaya kwa kufanya kazi zake binafsi likiwamo suala la pikipiki ya magudurumu matatu (bajaj) anayomiliki kwa sasa ikiwa ni mpango alioutekeleza kupitia changamoto ya mwenye ulemavu aliyefika ofisi hapo kuomba msaada.

“Ametumia mali za ofisi vibaya, amechukua mali za ofisi na kuzipeleka nyumbani kwake ikiwemo Kabati, viti vya ofisi na kuvihamishia nyumbani kwake na kamati tendaji ilipomuhoji alikiri kuvichukua vitu hivyo na kudai kwamba sio mali za Chawata,” alisema.

Pia Katibu huyo mtendaji alisema kikao cha Kamati ya Utendaji ya mkoa, kimekuwa kikizuiliwa na Mwenyekiti  huyo kufanyika kwa vikao ili kutoa taarifa za mapato na matumizi tangu mwaka jana.

“Nimejaribu kumshauri tuitishe kikao, lakini amekuwa akikataa na sababu za kukataa hazikuwa za msingi, jambo ambalo wajumbe liliwakwaza,”alisema.

Mjumbe wa Chawata wilaya ya Siha Yohana Orio, “Huu ni mwaka wa tano tangu tuchaguliwe uongozi wa Chawata wilaya na mkoa, kuna wajumbe walitafuna fedha zilizochangwa kwa ajili ya kuwekwa kwenye benki, hakuna hatua alizozichukua hadi sasa”alisema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chawata wilaya ya Rombo Veronica Swai, “Yeye amekuwa chanzo cha mgogoro wa kituo cha watoto yatima wilayani kwangu, wamekuwa wakishirikiana na Afisa Ustawi wa Wilaya ya Rombo hali ambayo imesababisha mfadhili aliyekuwa akiwafadhili watoto wenye ulemavu kujiondoa kuwasaidia watoto hao.”

Kaimu Mwenyekiti Chawata mkoa wa Kilimanjaro Barnaba Gwilla, alisema uamuzi wa  kuwasimamisha uongozi viongozi hao umekuja kufuatia kuwepo kwa malalamiko yaliyotolewa na wajumbe wa mkutano huo, dhidi ya Mwenyeiti huyo.

Gwilla alisema, Mwenyekitu huyo amekuwa akituhumiwa kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo matumizi mabaya ya fedha za michango inayotolewa na wadau,  wananchi  pamoja  wanachama, kutosoma mapato na matumizi ya fedha za michango mbalimbali ya inayotolewa na wahisani.

“Kuanzia leo aliyekuwa Mwenyekiti wa Chawata mkoa wa Kilimanjaro Kawawa Mwachitiku, tumemsimamisha uongozi, pamoja na makamu Mwenyekiti Chawata Bazil Lemunge na Katibu wa Chawata wilaya ya Rombo Getruda Kimario, wamekuwa wakienda kila ofisi na kuomba fedha kwa kutumia jina la chama chetu Chawata,”alisema Gwilla.