BAMAKO,MALI
VIONGOZI wa Afrika Magharibi wameongeza shinikizo dhidi ya kundi la wanajeshi waliotwaa madaraka nchini Mali kwa sasa wakilitaka jeshi hilo limuachie Rais Ibrahim Boubacar Keita na kumkubalia arudi madarakani.
Hayo yanajiri siku chache baada ya kiongozi huyo kulazimishwa kujiuzulu na wanajeshi hao waliompindua.
Viongozi wa mataifa ya Shirika la mataifa ya Afrika Magharibi ECOWAS pia walitaka kuweko na jeshi la kando wakisema Keita anastahili kukubaliwa aendelee kuongoza katika miaka yake mitatu iliyobakia.
Keita mwenye umri wa miaka 75 pamoja na Waziri wake mkuu bado wamezuiliwa na jeshi hilo katika kambi ya jeshi ya Kati.
ECOWAS ilisema jeshi hilo ndilo lililo na dhamana ya usalama wa Keita na maofisa wengine wa Serikali wanaozuiliwa.
Umoja wa Mataifa na Ufaransa wametaka hali ya utulivu na kuheshimiwa kwa sheria nchini Mali.