NA KHAMISUU ABDALLAH

VIONGOZI wa dini imeelezwa kuwa wana nafasi kubwa ya kuishawishi jamii katika ulinzi wa mtoto ili kumuepusha kuingia katika ndoa za umri mdogo.

Kauli hiyo ilitolewa na mwakilishi wa Shirika la Kimataifa la Save the Children Zanzibar, Amanda Procter katika mjadala wa siku moja uliozungumzia ndoa za umri mdogo kwa watoto uliowashirikisha viongozi wa dini katika ukumbi wa Zanzibar Beach Resort Mazizini.

Alisema ikiwa viongozi wa dini watachukua nafasi kusaidia kutoa elimu, hivyo kwa kiasi kikubwa wataokoa kundi la watoto wanaoolewa wakiwa katika umri mdogo.

Aidha alisema viongozi wa dini ni watu walio mstari wa mbele kusaidia watu kuwa na maadili bora na kufanya maamuzi yanayoendana na matakwa ya kiimani. 

Alisema, watoto wa miaka 15 wanahitaji elimu zaidi na wazazi kufahamu kuwa kumuozesha mtoto chini ya umri mdogo ni kumsabishia madhara kimwili na kiakili.

Aidha alisema utafiti mdogo uliofanywa na shirika la UNICEF unaonesha kuwa kwa Zanzibar asilimia 3.5 ya watoto wanaolewa chini ya umri wa miaka 15, watoto wanaojifungua chini ya umri huo ni asilimia mbili huku wanaoolewa chini ya umri wa miaka 18 ni asilimia 18.

Hata hivyo, alibainisha kuwa shirika lao limepata mafanikio ikiwemo kuchukua jitihada kwa kuanzisha programu ya malezi bila ya ukatili katika wilaya ya Kusini na kuwafikia wazazi 3,000 sambamba na kuwajengea uwezo watoto katika masuala ya ulinzi na kuunga mkono vituo vya mkono kwa mkono katika vituo vyote vya Zanzibar.

Kwa upande wa Ofisa wa Haki za Watoto na Utawala wa shirika hilo Dickson Megera, alisema mimba za umri mdogo ni changamoto kubwa kwa Zanzibar.

Alisema, ndoa ni kitu chema na msingi, lakini ni lazima kifanywe kwa wakati sahihi pamoja na kuangalia maslahi kwa mtu anaeolewa na anaeowa kwa familia zao.

Hata hivyo, alisema kitaalamu, kiafya na makubaliano ya jamii nyingi duniani mtoto mwenye umri wa miaka 18 ndio umri ambao unaonekana kuwa mtoto amekuwa kiakili.

Akifungua mjadala huo Katibu wa Mufti Khalid Ali Mfaume alisema ndoa za umri mdogo zina madhara makubwa kwa mtoto ikiwemo kuathirika kwa mfumo mzima wa maisha.