KAMPALA,UGANDA

ASILIMIA  80 ya vipimo vyote vya ugojwa wa COVID-19 barani Afrika vinafanyika katika nchi kumi pekee jambo ambalo linaonyesha udhaifu mkubwa katika vipimo vya corona barani humo.

Idadi ya walioambukizwa corona barani Afrika inaongezeka na inatarijiwa kufika milioni moja wiki hii huku wataalamu wakionya kuwa idadi ndogo ya vipimo katika nchi ni jambo linaloashiria kuwa maambukizi ni makubwa kuliko inavyoripotiwa.

Taarifa zinasema baadhi ya nchi barani Afrika ni masikini au zinakumbwa na vita vya ndani na hivyo hazina uwezo wa kupima huku baadhi ya nchi zikiwa zinaficha ukweli kwa kuhofia kuwa mifumo duni ya afya katika nchi hizo itaangaziwa kimataifa.

Kwa mujibu wa Daktari John Nkengasong, mkuu wa Vituo vya Kudhibiti Magonjwa Afrika (Africa-CDC) alisema nchi kumi za Afrika ambazo zilifanya asilimia 80 ya vipimo vya corona barani humo ni Afrika Kusini, Misri, Nigeria, Ghana, Morocco, Kenya, Ethiopia, Rwanda, Uganda na Mauritius.

Alisema kila moja ya nchi hizo ilifanikiwa kufanya vipimo zaidi ya 200,000 vya corona.

Nkengasong alisema Africa CDC inajitahidi kuzisaidia nchi kadhaa kuimarisha uwezo wa kupima corona.