NA HAJI NASSOR, PEMBA

MUFTI Mkuu wa Zanzibar sheikh Saleh Omar Kaabi, amesema ujio wa vyama vingi vya siasa nchini, haukuletwa kwa malengo ya kubaguana, kukashifiana na kuripuana bali ni kuchapuza maendeleo kwa wananchi wote bila ya ubaguzi.

Alisema, sasa imekuwa ni kero, kebehi, matusi, kubaguana, kuacha kuzikana na kuondoleana heshima kutokana na mfumo wa vyama vingi, wakati hilo sio lengo lake kama wengine wanavyofanya.

Akizungumza na masheikh na maimamu wa miskiti ya Pemba, kwenye mkutano wa siku moja uliofanyika Gombani Chake Chake, alisema lazima wananchi waondokane na mawazo finyu juu ya uwepo wa vyama vingi vya siasa.

Mufti huyo alisema, haifai na wala isisimamiwe na miongoni mwa waumini na viongozi wa dini, kubaguana na kuacha kuzikana kwa sababu ya kukosana kwao kwenye siasa.

Alieleza kuwa, moja ya kazi ya viongozi hao wa dini ni kuhakikisha wanakaa na kuwaeleza wafuasi wao kila wakati, juu ya umuhimu wa kuishi kwa kuheshimiana huku amani ikitawala katika maisha yao na siasa iwe chanzo cha kuwabagua, kiimani.

“Nyinyi masheikh na maimamu mnao wajibu wa kuwatuliza wafuasini wenu, wasiwe chanzo cha uvunjifu wa amani, unaotokana na siasa, maana lengo la hii ni kuongeza kasi ya maendeleo,’’alieleza.

Aidha Mufti mkuu huyo wa Zanzibar, sheikh Saleh Omar Kaabi, alisema hakuna haja ya kuivuruga amani iliyopo na kuzalisha migogoro, kwani zipo njia kadhaa zinazoshauriwa kufanya inapotokezea siutofahamu.