ILIKUWA miaka ikapita taratibu, na sasa si zaidi ya miezi iliyobakia kabla Watanzania kupiga kura katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 28, 2020.

Wakati tukisubiri kufanya maamuzi yahusuyo mustakbali wa taifa letu, kwa upande wa Jamhuri ya Muungano wa Tanznaia na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ni vyema tukumbushane umuhimu wa kuiengaenga tunu ya amani tuliyonayo.

Tukiachia Tanzania ambayo iko katika awamu ya tano ya uongozi, Zanzibar imeshaongozwa na marais saba kwa vipindi tafauti, wengine wakishindwa kumaliza miaka mitano kutokana na sababu mbalimbali, na baadhi wakishika hatamu kabla ya mageuzi yaliyoleta mfumo wa vyama vingi.

Ni dhahiri kuwa, kama ilivyozoeleka katika chaguzi zilizopita chini ya mfumo wa vyama vingi, uchaguzi wa mwaka huu pia umeanza kuonesha kwamba utakuwa na presha kama ule wa miaka mingine iliyopita.

Kama kawaida ya chaguzi zote, tunaelewa kwamba wakati wa mikutano ya kampeni, wagombea hutumia nguvu nyingi na sauti zinazofika mbali kushindanisha sera, ili kuwavutia wapiga kura wawape ridhaa.

Ingawa kila mgombea urais ana imani kubwa ya kushinda kwa mujibu wa maelezo waliyoyatoa wakati na baada ya kupitishwa na vyama vyao, lakini ni vyema tukachukua fursa hii kuwakumbusha kwamba katika mashindano yoyote yale, daima mshindi anakuwa mmoja tu.

Majigambo, mbwembwe, nyimbo na kila aina ya vituko kabla ya mechi, huwa ni mbinu tu za kuwavuruga kisaikolojia wapinzani ili wapate hofu na kutoka mchezoni, na hivyo kuwapa mwanya washambuliaji wa timu pinzani kufunga magoli.

Lakini mwisho wa mchezo, muamuzi anapopuliza firimbi ya kuzitoa timu dimbani, aliyetumia vyema dakika 90 kwa kupachika magoli mengi, au japo moja kwa bila, ndiye anayehesabiwa kuwa mshindi kwa mujibu wa sheria na kanuni.

Kushinda au kushindwa, ni miongoni mwa kanuni za mchezo na timu isipokubaliana na msamiati wa kupoteza, ikalazimisha ushindi tu, huitwa si mshindani.

Kwa muktadha huo na kwa mnasaba wa shughuli ya uchaguzi ni wazi kanuni hii itachukua nafasi yake baada ya mwamuzi ambayeni Tume ya Uchagui kumaliza mpambano na kutangaza matokeo.

Baada ya yote hayo, sote tuelewe kuwa, mgombea yeyote atakaetangazwa na tume kwamba ameshinda, atakuwa mtumishi wa Watanzania na Wazanzibari wote na hatakuwa wa chama alichopitia kugombea nafasi hiyo.

Nasaha zetu kwa wananchi ni kwamba mara baada ya tume kutangaza washindi wa urais, wabunge, wawakilishi na madiwani, tuzingatie amani na usalama katika kusherehekea na kupongezana ili taifa letu liendelee kuwa kisiwa cha amani na utulivu.

Uchaguzi bila kugombana, uchaguzi bila ya kujitokeza viashiria vya uvunjifu wa amani inawezekana, tujiandae kuyapokea na kuyakubali matokeo hata kama yatakuwa machungu kwa wengine, ndio ushindani huo.